MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE ANG'AKA ASILIMIA 10 YA MAKUNDI MAALUM KUTOWAWEZESHA WASICHANA BALEHE AAGIZA KUPEWA HARAKA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday 12 October 2023

MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE ANG'AKA ASILIMIA 10 YA MAKUNDI MAALUM KUTOWAWEZESHA WASICHANA BALEHE AAGIZA KUPEWA HARAKA

Kamati ya Bunge ya maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake, Watoto na makundi maalum imeiagiza halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kuhakikisha inatekeleza takwa la kisheria kwa kutoa mikopo kwa vikundi ili kuvikwamua kiuchumi.
Naibu Waziri, ofisi ya Waziri mkuu sera, Bunge na uratibu, Ummy Nderiananga akikagua bidhaa zinazozalishwa na wasichana kwenye vikundi vyao vya kiuchumi


NA PASCHAL MALULU-HUHESO DIGITAL NA HUHESO FM

Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Stanslaus Nyongo ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki leo Oktoba 12, 2023 katika ziara ya kukagua vikundi vya wasichana wajasiliamali wenye miaka 15-25 ambao wanajishughulisha na shughuli za kujiingizia kipato.

 

Amesema halmashauri katika mapato yake ya ndani inapaswa kutoa asilimia kumi ya mapato yake ili kutoa mikopo kwa wanawake asilimia 4, vijana asilimia 4 na walemavu asilimia 2 kwa mujibu wa sheria kwa kila halmashauri kufanya hivyo.

 

Nyongo amesema endapo Watoto wa kike wakipewa mitaji ya kujiendeleza kiuchumi wataepukana na tabia mbaya ambazo zimekuwa chanzo cha kueneza maambukizi ya VVU kwani wanakumbana na vishawishi ambavyo wanashindwa kuvikwepa hivyo serikali inapambana kila namna kuhakikisha wasichana ambao wapo kwenye hatari ya maambukizi wanawezeshwa kikamilifu.

 

“halmashauri tuhakikishe mabinti hawa wanapata mitaji kwa kwa wakati kwani inawarudisha nyuma wanapokuwa wanajilipia wenyewe pango la nyumba tukiwasaidia mikopo watamudu gharama zote, pia tumewasikia wanaomba vyerehani tuhakikishe tunawapatia tunapokuja mwakani tukute mmewawezesha”. Amesema Nyongo.

 

Mwenyekiti kamati ya Bunge ya maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake, watoto na makundi maalum Stanslaus Nyongo ambaye pia ni mbunge wa Maswa Mashariki


Kwa upande wake naibu Waziri, ofisi ya Waziri mkuu sera, Bunge na uratibu, Ummy Nderiananga amesema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inawathamini vijana hivyo anatoa fedha kwa ajili ya mikopo ili kujikwamua kiuchumi.

 

Naibu Nderiananga pia amewataka viongozi wa serikali ndani ya wilaya ya Kahama kupitia kwa katibu tawala na mkuu wa wilaya kuhakikisha wanakwenda kwenye vikundi vya wasichana hao ili kuwasikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili.

 

“Katibu tawala twendeni tukawasikilize hawa mabinti mnaona kamati ya Bunge imetoka Dodoma kuja mpaka waliopo haijakaa ofisini halafu mabinti ndio waende Dodoma tuwasikilize na kutatua changamoto zao”.

 

Hata hivyo kwa upande wake msimamizi wa shughuli za DREAMS mradi wa Epic-fhi360 Mkoa wa Shinyanga, Agnes Junga amesema kuwa wao kama watekelezaji wa miradi ya vikundi hivyo wamekuwa wakiwafuatilia mabinti hasa walio na maambukizi ya VVU kwa kuwafuata walipo na kuwapa ushauri nasaha na kuwaunganisha katika vikundi.

 

Bi. Junga amesema katika vikundi hivyo wamekuwa wakiwawezesha kupata mitaji sambamba na kuwafundisha ujuzi mbalimbali ambao unawasaidia kujikwamua kiuchumi.

 

“Tumekuwa tunawaunganisha katika vikundi na kuwawezesha mbinu mbalimbali ambazo ni Pamoja na ufundi cherehani, Ujasiliamali wa kutengeneza vitu kama sabuni, mkaa mbadala na uchomaji matofali” amesmea Junga

 

Aidha Kamati ya Bunge, maendeleo ya Jamii, jinsia, wanawake, Watoto na makundi maalum imefanya ziara ya kuvitembelea vikundi vyote ambavyo vinajishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi sambamba na kutatua changamoto zinazowakabili.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso