SHUGHULI ZA UCHIMBAJI MADINI ZATAJWA KUKATISHA MATUMIZI YA ARVs-KAHAMA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday 14 October 2023

SHUGHULI ZA UCHIMBAJI MADINI ZATAJWA KUKATISHA MATUMIZI YA ARVs-KAHAMA


Imeelezwa kuwa shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu katika migodi midogo wilayani Kahama mkoani Shinyanga zinakwamisha juhudi za ufuatiliaji wa matumizi ya dawa za kufubaza Ukimwi (ARVs) kwa wenye maambukizi.



NA PASCHAL MALULU-HUHESO DIGITAL


Hayo yameelezwa na DACC, Silvester Hery wakati akisoma ripoti mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Watoto na makundi maalum wakati wa ziara yake katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga iliyofanyika Oktoba 12, 2023.


DACC Hery amesema katika ufuatiliaji wa maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi kwa mwaka 2020 hadi Septemba 2023 jumla ya maambukizi zaidi ya Elfu 41 yamepatikana ambapo wasichana ni Elfu 19 ambao wamekuwa wakiwezeshwa kiuchumi ili kuzuia maambukizi mapya.


Amesema katika ufuatiliaji wa kuhakikisha wanatumia dawa za ARVs inavyotakiwa wamekuwa wanapata changamoto kuwapata kwani wanajishughulisha na ujasiliamali katika migodi ya uchimbaji madini hivyo wanahama hama na kutotumia dawa hizo.


“Wilaya Kahama ina migodi mingi ya uchimbaji asilimia kubwa tunaowaibua kuwa na maambukizi ya VVU katika ufuatiliaji wetu wa matumizi ya dawa hatuwapati kutokana na kuwa wanahama hama kutokana na shughuli wanazofanya hiyo ndio changamoto inayotukabili sisi kama watoa huduma na wafuatiliaji na waibuaji wa VVU”.


Kwa upande wake msimamizi wa shughuli za DREAMS mradi wa Epic-fhi360 Mkoa wa Shinyanga, Agnes Junga amesema pindi wanapowabaini wenye maambukizi ambao ni mabinti kwa kuwafuata huko waliko wamekuwa wakiwawezesha kiuchumi kwa kuwapa mitaji kwenye vikundi na kuwafundisha mbinu mbalimbali za kiuchumi.


Bi. Junga ameieleza kamati kuwa vikundi vya wanawake na wasichana vinavyojishughulisha na ujasiliamali kwa Manispaa ya Kahama vipo chini ya shirika la Huheso foundation ambalo linawawezesha mabinti katika ufundi mbalimbali ikiwemo cherehani, ufumaji vitambaa.


Akizungumza mara baada ya kuvitembelea vikundi vya wasichana na wanawake Kata za Kagongwa, Mhongolo na Majengo, mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge Stanslaus Nyongo amelipongeza shirika la Huheso foundation kwa uwezeshaji huo huku akishauri kuwa mbali na kuwawezesha kiuchumi mabinti hao ufuatiliaji uongezwe nguvu.


Amesema changamoto zilizoelezwa wasichana hao ikiwemo maeneo ya kufanyia shughuli zao, Mitaji na vifaa vya kujifunzia kama cherehani nguvu kubwa iwekezwe ili kuhakikisha wanapata kwa wakati ili kuwanusuru na tabia potofu ambazo zinawarudisha nyuma.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso