NA NEEMA NKUMBI HUHESO DIGITAL KAHAMA
Juni 28, 2025 – Kahama
Jumla ya wagombea 16 wa nafasi ya ubunge kutoka katika majimbo matatu ya Wilaya ya Kahama wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo leo, Juni 28, 2025, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama, Andrew Chatwanga, amesema kati ya wagombea hao, wanane (8) wanatoka Jimbo la Kahama Mjini, sita (6) kutoka Jimbo la Msalala, na wawili (2) kutoka Jimbo la Ushetu.
Chatwanga amewataka wana CCM wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali kufuata utaratibu wa kuchukua fomu kama ulivyoelekezwa na chama, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia kanuni na miongozo ya chama katika mchakato huo wa ndani.
Miongoni mwa waliowasilisha nia ya kugombea ubunge ni Salum Ismail Salum, ambaye ametangaza nia ya kuwania ubunge katika Jimbo la Kahama Mjini, Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Salum amesema msukumo mkubwa kwake umetokana na uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuwaamini vijana na kuwapa nafasi katika uongozi wa nchi.
Aidha, Salum amesema moja ya sababu kubwa zilizomvutia kuwania nafasi hiyo ni changamoto ya miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Kahama, hususan maeneo yenye viwanda vya kuchakata mpunga maarufu kama Malunga, ambayo hayako katika hali inayoendana na nafasi ya wilaya hiyo kuwa miongoni mwa maeneo yanayochangia pato kubwa la taifa.
“Wilaya yetu ya Kahama inachangia mapato mengi sana, lakini hali ya uchumi na miundombinu haionyeshi uwiano na mchango huo mkubwa. Tunahitaji kusimamia maslahi ya wananchi na kuimarisha barabara za viwandani ili kuchochea uchumi wa ndani,” amesema Salum.
Ameongeza kuwa maboresho ya barabara katika maeneo ya mashine za kuchakata mpunga yataongeza tija kwa wawekezaji, kurahisisha usafirishaji wa mazao na kukuza pato la taifa kwani mchele unaochakatwa Kahama unauzwa hadi nje ya nchi.
Mbali na hayo, Salum amesisitiza kuwa pia analenga kusimamia usawa wa kijinsia, akitoa mfano wa Rais Samia kuwa ni kielelezo thabiti kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa uongozi licha ya vikwazo vya kijamii na kimtazamo.
“Kama tulivyoshuhudia kwa Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, wanawake wanaweza kuongoza na kuleta mageuzi makubwa. Tunapaswa kuondoa dhana ya ubaguzi wa kijinsia na kutoa nafasi sawa kwa wote,” amesema.
Mchakato wa uchukuaji fomu unaendelea katika wilaya hiyo huku hali ya kisiasa ikizidi kupamba moto, wagombea mbalimbali wakijitokeza kwa matarajio ya kulitumikia taifa kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment