Vijana nchini wametakiwa kuipenda na kuilinda nchi yao, kudumisha amani na kuwa wazalendo ili kuchangia maendeleo ya taifa.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi, wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana uliofanyika katika Chuo cha Mipango, mkoani Dodoma.
Waziri Katambi amesema serikali itaendelea kuwaunganisha vijana kupitia majukwaa mbalimbali kwa lengo la kusikiliza maoni yao na kutatua changamoto zinazowakabili.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupitia mikopo na programu mbalimbali za kuwawezesha kiuchumi.
"Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara yenye dhamana ya vijana itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto za vijana pamoja na kuweka mikopo inayolenga kuwawezesha kiuchumi," amesema Katambi.
Aidha, amewahimiza vijana kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.
Katika hatua nyingine, Waziri Katambi amewataka vijana walioshiriki kongamano hilo kutumia maarifa waliyopata kutoa maoni kuhusu maboresho ya Dodoso la Baraza la Vijana, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana Toleo la 2024, elimu ya uraia, uzalendo, kujitolea pamoja na fursa za kiuchumi zinazopatikana katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na nchini kwa ujumla.

No comments:
Post a Comment