AFCON 2027: TANZANIA KUANZA 'KUJIBRAND' KIVINGINE, SHILINGI TRILIONI 1.2 KUAMSHA UCHUMI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 3 April 2026

AFCON 2027: TANZANIA KUANZA 'KUJIBRAND' KIVINGINE, SHILINGI TRILIONI 1.2 KUAMSHA UCHUMI




Serikali imetangaza rasmi kuanza kwa kampeni kabambe ya kuibeba taswira ya nchi (branding) kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), huku ikilenga kuvuna mabilioni ya fedha kupitia uwekezaji wa zaidi ya Shilingi trilioni 1.2.


Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amebainisha kuwa mchakato huo utaanza wakati wowote kuanzia sasa ili kutia hamasa ndani na nje ya nchi, akisisitiza kuwa katika mwezi Aprili, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) litaanza kuonesha njia ya namna Tanzania itakavyovuna fursa hizo.


Msigwa anafananisha mashindano hayo na "bidhaa" ambayo ikichangamkiwa itachangamsha uchumi, akitolea mfano nchi ya Morocco iliyovuta takriban Dola bilioni 1.9 kupitia uenyeji. Ili kufikia mafanikio hayo, Serikali imeshachukua hatua madhubuti ikiwemo kulipa ada ya ushiriki ya Dola milioni 30, nje ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa katika vituo vya Dar es Salaam, Zanzibar, na Arusha.


Wadau wa uchumi na michezo wameipokea hatua hii kwa mtazamo chanya, wakibainisha kuwa AFCON 2027 itakuwa na athari za moja kwa moja katika kukuza Pato la Taifa (GDP). Uchambuzi wa kiuchumi unaonesha kuwa sekta ya utalii wa michezo itakuwa na mnyororo mrefu wa thamani; kuanzia usafirishaji, malazi, hadi vyakula. Uwepo wa mashindano haya unatarajiwa kuongeza mzunguko wa fedha za kigeni na kuimarisha thamani ya Shilingi kutokana na ujio wa maelfu ya wageni.


Kwa upande wa wajasiriamali wadogo, Waziri Mkuu kupitia kwa Dkt. Mwigulu Nchemba, ameweka wazi mkakati wa Serikali wa kuandaa mazingira wezeshi. Hii ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kuweka taa zitakazowezesha biashara kufanyika saa 24, pamoja na kutenga maeneo maalum ya biashara karibu na viwanja vya mazoezi na mechi. Lengo ni kuhakikisha huduma na bidhaa za asili za Kitanzania zinawafikia wageni kwa urahisi, jambo litakaloinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja.


Huu ni ushirikiano wa kihistoria wa "Pamoja" kati ya Tanzania, Uganda, na Kenya, ambapo Tanzania imepania kuonesha ulimwengu utajiri wake wa kitamaduni na vivutio vya utalii. Kama wadau wanavyofafanua, uwekezaji huu ni zaidi ya soka; ni daraja la kuunganisha fursa za kibiashara na kuitangaza Tanzania kama kitovu kipya cha michezo na uwekezaji barani Afrika.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso