Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetangaza neema ya kiuchumi baada ya kusajili miradi 177 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, kuanzia Januari hadi Machi. 

Miradi hiyo inatarajiwa kuleta mtaji wa Dola za Marekani bilioni 1.122, ambayo ni zaidi ya Shilingi trilioni 2.9, na inakadiriwa kuzalisha ajira mpya 19,750 nchini. 

Mkurugenzi wa TISEZA, Gilead Teri, amebainisha kuwa kasi ya uwekezaji imekua kwa viwango vya kihistoria ambapo usajili wa miradi umeongezeka kutoka miradi 252 mwaka 2021 hadi kufikia miradi 927 mwaka 2025. 

Vilevile, mitaji kutoka nje imepaa kutoka Dola bilioni 3.7 hadi Dola bilioni 11.08 katika kipindi hicho, jambo linalovunja rekodi kila mwaka licha ya nchi kupitia vipindi vya uchaguzi.

Sekta ya uzalishaji viwandani inaendelea kuwa injini kuu ya uwekezaji ikishikilia asilimia 51 ya miradi yote na asilimia 63 ya ajira zinazotarajiwa kuzalishwa. 

Sekta nyingine za kimkakati zinazofanya vizuri ni pamoja na utalii, ujenzi wa majengo ya biashara, miundombinu ya uchumi, na kilimo. Katika hatua ya kupongezwa, asilimia 57.6 ya miradi hiyo inamilikiwa na Watanzania wenyewe, ikiwa ni utekelezaji wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wazawa wanakuwa sehemu ya uchumi wa nchi. 

Kwa sasa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani inaendelea kuongoza kwa kuvuta uwekezaji mkubwa zaidi, huku nchi 38 zikiwa tayari zimeshasajili miradi nchini.

Aidha Serikali imefungua ukurasa mpya katika sekta ya madini baada ya kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na viongozi wa kampuni ya Liaoning Fangda Group kutoka China, ambayo ni miongoni mwa makampuni makubwa duniani katika sekta ya viwanda na madini. 

Mazungumzo hayo yaliyoongozwa na Kamishna wa Madini, Dk. AbdulRahman Mwanga, yamejikita katika utafutaji, uchimbaji, na uongezaji thamani wa madini kupitia teknolojia za kisasa. 

Dk. Mwanga amesisitiza kuwa Tanzania imeunda mazingira thabiti na rafiki kwa uwekezaji ili kuhakikisha rasilimali za madini zinachangia moja kwa moja katika ukuaji wa viwanda na maendeleo ya taifa.

Makamu Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Ao Xinhua, ameipongeza Tanzania kwa kuwa na utulivu wa kisiasa na sera thabiti zinazohamasisha uongezaji thamani wa madini kabla ya kusafirishwa nje. 

Liaoning Fangda inaiona Tanzania kama mshirika mkuu wa kimkakati barani Afrika, hususan katika viwanda vinavyotegemea madini ya chuma na uchakataji wa teknolojia ya juu. Ushirikiano huu unatarajiwa kuharakisha ukuaji wa uchumi na kutengeneza ajira zenye ubora wa juu kwa Watanzania, huku pande zote mbili zikiendelea na mashauriano ya kitaalamu ili kutathmini miradi mahsusi itakayotekelezwa.