NA SHEILA KATIKULA- MWANZA
JESHI la Polisi mkoani Mwanza limeeleza kuwa litaimarisha kwa kiasi kikubwa ulinzi na usalama katika kipindi hiki hiki cha sikukuu ya Pasaka, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanasherehekea kwa amani na utulivu bila hofu ya matukio ya uhalifu.
Hatua hiyo imekuja sambamba na kuongeza doria katika maeneo mbalimbali ya mijini na vijijini, hususan katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama masoko, vituo vya usafiri, nyumba za ibada na maeneo ya burudani.
Aidha, jeshi hilo limeeleza kuwa limejipanga kikamilifu kushughulikia vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani, ikiwa ni pamoja na uhalifu wa kawaida na makosa ya barabarani.
Maafisa na askari wa usalama wameelekezwa kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha wanatoa huduma kwa wananchi kwa haraka na kwa ufanisi katika kipindi chote cha sikukuu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Willibroad Mutafugwa, amesema kuwa mafanikio ya kudumisha amani yanategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano kati ya jeshi la polisi na wananchi.
Amebainisha kuwa elimu inayotolewa kupitia mikutano ya hadhara na kampeni mbalimbali imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya usalama.
Kamanda Mutafugwa amewapongeza wananchi kwa kuendelea kuitikia wito wa kushiriki katika mikutano ya uhamasishaji na kuzingatia maelekezo wanayopewa, jambo ambalo limechangia kupungua kwa matukio ya uhalifu katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo.
Amesema mwitikio huo unaonesha kuwa wananchi wana dhamira ya dhati ya kulinda amani katika jamii zao.
Pamoja na mambo mengine Kamanda Mutafungwa, amewahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa wakati kuhusu vitendo vyovyote vinavyotia shaka ili viweze kushughulikiwa mapema kabla havijaleta madhara makubwa.
Amesisitiza kuwa usalama ni jukumu la kila mmoja, na kwamba bila ushirikiano wa karibu, juhudi za jeshi la polisi haziwezi kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Katika kuhakikisha usalama wa barabarani, jeshi la polisi pia limeweka mikakati maalum ya kudhibiti ajali zinazoweza kujitokeza wakati wa sikukuu, ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto na kuhimiza madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Hatua hizi zinalenga kupunguza ajali ambazo mara nyingi huongezeka wakati wa misimu ya sikukuu.
Vilevile, wazazi na walezi wametakiwa kuwa makini na watoto wao katika kipindi hiki cha sikukuu, hususan wanapokuwa katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu, ili kuepuka matukio ya kupotea au madhara mengine yasiyotarajiwa.
Kwa ujumla, Kamanda Mutafugwa amesisitiza kuwa jeshi la polisi litaendelea kuwepo karibu na wananchi katika kipindi chote cha Pasaka, na ametoa wito kwa kila mmoja kusherehekea kwa amani, kuepuka vitendo vya uvunjifu wa sheria, na kudumisha mshikamano ili kuhakikisha mkoa wa Mwanza unaendelea kuwa salama wakati wote.


No comments:
Post a Comment