BEI YA NYAMA YAZIDI KUPANDA JIJINI DODOMA, NG'OMBE WAPUNGUA KWENYE MINADA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday 6 January 2023

BEI YA NYAMA YAZIDI KUPANDA JIJINI DODOMA, NG'OMBE WAPUNGUA KWENYE MINADA


Bei ya nyama ya ng'ombe kwenye baadhi ya mabucha katika jijini la Dodoma imepanda kutoka Sh7,000 hadi Sh10,0000 kwa kilo huku moja sababu ikitajwa kuwa ni uhaba wa ng’ombe minadani mkoani Dodoma.


Wakizungumza na Mwananchi leo Alhamisi ya Januari 5, 2023 jijini hapa, wamiliki wa mabucha wamesema kwa sasa biashara ni mbaya kwani minada ya Kizota na Msalato mkoani Dodoma kuna uhaba wa ng’ombe na hata wakipatikana bei zipo juu.


Shaban Juma, mmiliki wa mabucha ya Shebby, amesema licha ya kuadimika, lakini ng'ombe mwenye kilo 60 anauzwa kwa zaidi ya Sh700,000 hali inayowapa wakati mgumu.


“Tumekubaliana kupandisha bei ili na sisi tupate kitu kidogo, lakini biashara imekuwa mbaya kwetu, wanunuzi wa nyama wamekuwa wachache,” amesema Juma.


Amesema kwa sasa wamekuwa wakilazimika kuwafuata wafugaji vijijini katika maeneo ya Bahi na Chemba ambao pia wanauza kwa gharama kubwa.


Francis John, mmiliki wa mabucha ya Francis amesema sababu ya kuadimika kwa ng'ombe ni kutokana na wafugaji wengi kusafirisha mifugo kwenda Dar es Salaam.


“Bei imepanda pia kutokana na kupanda kwa gharama za usafirishaji kutoka vijijini hadi kwenye minada, zamani ilikuwa ni kuswaga tu mpaka machinjio au minadani.


“Sasa hivi waswagaji wanataka mpaka Sh20,000 kwa ng’ombe mmoja,” amesema John.


Kwa upande wake, muuzaji wa nyama katika eneo la Sabasaba, Ramadhan Elius amesema awali walikuwa wakiuza kwa Sh6,000 mpaka Sh7,000 lakini sasa imepanda hadi Sh9,000.


“Kimsingi tunakoelekea huenda ikapanda zaidi kwani wafanyabiashara wa nyama wanalalamikia ng'ombe kuadimika na hata wakiwapata wanakuwa hawana ubora unaotakiwa,” amesema.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso