.jpg=w72-h72-p-k-no-nu)
Vijana mkoani Dodoma wamehamasishwa kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo kwa kujikita katika kuongeza thamani ya mazao kupitia matumizi ya teknolojia, zana, na mashine za kisasa ili kukuza ajira, kuongeza kipato, na kuchochea ukuaji wa viwanda vidogo.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana yaliyolenga kuongeza tija katika kilimo na viwanda, Kaimu Meneja wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Dodoma, Justine Kahemela, alieleza kuwa mafunzo hayo yalihusisha vijana 53 chini ya ufadhili wa Muungano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA) kupitia Mradi wa Agra wa Ajira kwa Vijana katika Chakula na Kilimo (YEFFA).
Alisema kupitia mradi huo, SIDO imejikita katika kuwajengea uwezo vijana ili watumie mitambo na mashine bora zitakazowezesha ufanisi mkubwa kuanzia hatua za uzalishaji, uvunaji, uhifadhi, usindikaji, ufungashaji, hadi utafutaji wa masoko, jambo litakalowasaidia kuachana na tabia ya kuuza mazao ghafi na badala yake kupata faida kubwa kupitia mnyororo wa thamani.
Kahemela alisisitiza kuwa fursa katika mnyororo wa thamani wa kilimo ni pana sana na zinajumuisha maeneo ya ukusanyaji, usafirishaji, uwekaji wa nembo, ubunifu wa bidhaa, na ushirikiano wa karibu kati ya wakulima, wasindikaji, wazalishaji wa mashine, na wafanyabiashara ili kujenga uchumi thabiti wa viwanda vidogo mkoani humo.
Mtazamo huo uliungwa mkono na mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Ayub Rioba, aliyeeleza kuwa mafunzo hayo yamewapa mwanga mpana na uelewa wa kina kuhusu umuhimu wa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wakulima na mafundi ili kuimarisha shughuli za kilimo biashara na kujiletea maendeleo endelevu ya kiuchumi
No comments:
Post a Comment