MSIMAMO WA TANZANIA UN UNAPOPONGEZWA NA UPINZANI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 25 September 2026

MSIMAMO WA TANZANIA UN UNAPOPONGEZWA NA UPINZANI




Viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani nchini wameipongeza serikali kwa kueleza wazi msimamo thabiti wa Tanzania kuhusu siasa na diplomasia ya kimataifa, baada ya Makamu wa Rais kuwasilisha msimamo huo kwenye mkutano mkuu wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.



Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib, alieleza kuwa hotuba hiyo inaonyesha Tanzania ni nchi inayopenda haki, usawa na amani huku akitolea mfano wa msimamo wa nchi kusimama na kuwatetea wananchi wa Palestina.

Khatib aliongeza kuwa kupitia historia nzuri ya Tanzania katika kupigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika, uamuzi wa nchi kuwania kiti cha muda katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa utaleta tija kubwa na kulipatia bara la Afrika fursa ya kuwa na sauti ya pamoja katika masuala ya amani na usalama wa kimataifa.

Mtazamo huo uliungwa mkono na viongozi wengine wa vyama vya siasa akiwemo mgombea urais kupitia Chama Cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale, ambaye alieleza kuwa uamuzi wa kuwania kiti hicho unachangiwa na misingi imara ya amani, upendo na uzalendo uliopo nchini, huku akisisitiza kuwa usalama barani Afrika ni nguzo kuu ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Naye mgombea urais kupitia Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), Mwajuma Mirambo, alibainisha kuwa hali nzuri ya kisiasa ya ndani ya nchi ndiyo iliyochangia Tanzania kujitathmini na kuona ina uwezo wa kushika nafasi hiyo ya juu kidiplomasia, akisisitiza kuwa Afrika inapaswa kusimama pamoja ili kusimamia maslahi yake yenyewe.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Katibu Mkuu wa National League of Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, aliyeeleza kuwa hatua hiyo ni ishara wazi kwamba Tanzania iko imara kiuchumi na kidiplomasia katika nyanja za kimataifa.

Wachambuzi wa siasa na diplomasia nchini nao wameunga mkono hatua hiyo, wakisema inaleta heshima kubwa na fursa za kimkakati kwa taifa.

Mchambuzi wa masuala ya kimataifa, Leonard Soza, alikumbusha kuwa Tanzania imewahi kuhudumu katika baraza hilo mara mbili hapo awali, ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1975 hadi 1976 chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, na mara ya pili kuanzia mwaka 2005 hadi 2006 katika uongozi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Soza alieleza kuwa kupitia nafasi hiyo, Tanzania inapata fursa ya kipekee ya kujenga urafiki wa kimkakati na mataifa makubwa matano yenye viti vya kudumu katika baraza hilo, jambo ambalo linaweza kutumika kushawishi wawekezaji kuwekeza kwenye sekta za kipaumbele nchini sambamba na kusaidia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Mtazamo huo uliungwa mkono na aliyekuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Modest Mero, ambaye alieleza kuwa uzoefu wa nchi katika kuongoza kwa mafanikio miaka ya nyuma unatoa picha halisi kuwa Tanzania ina uwezo mkubwa wa kushinda na kuongoza tena kwenye awamu ijayo.

Naye mchambuzi wa siasa, Said Msonga, aliongeza kuwa uwepo wa Tanzania katika baraza hilo utasaidia kutoa sauti thabiti kwa nchi za ulimwengu wa tatu na wa pili ambazo mara nyingi hukosa jukwaa la kutosha la kusemea changamoto zinazowakabili katika majukwaa ya kimataifa, hatua itakayozidi kuimarisha nafasi ya nchi kama mbeba maono wa amani na maendeleo duniani.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso