Video: UKOSEFU WA MAJI YA UHAKIKA LUGELA, KAHAMA, NGAYIWA AITAKA KUWASA KUKAMILISHA HARAKA MRADI UNAOENDELEA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 29 September 2026

Video: UKOSEFU WA MAJI YA UHAKIKA LUGELA, KAHAMA, NGAYIWA AITAKA KUWASA KUKAMILISHA HARAKA MRADI UNAOENDELEA


Mbunge wa Kahama Mjini Benjamin Ngayiwa akizungumza na wananchi wa Lugela, kata ya Nyahanga, akizungumza na wakazi wa Lugela katika muendeleza wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.




KAHAMA


Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, ameendelea na ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, ambapo amefika Mtaa wa Lugela, Kata ya Nyahanga, Manispaa ya Kahama, na kukutana na changamoto ya ukosefu wa maji ya uhakika kwa wananchi.


Akizungumza katika mkutano huo, mkazi wa Lugela, Boaz Simon, amesema wananchi wamekuwa wakikabiliwa na adha ya kutafuta maji, huku baadhi yao wakilazimika kuchota maji kutoka maeneo ya chini na kuyapeleka maeneo ya mlimani.


Boaz amesema wananchi waliwahi kushirikiana katika kuchimba mitaro kwa ajili ya kupitisha mabomba ya maji, huku baadhi yao wakitumia fedha zao kugharamia uchimbaji huo, lakini wameshangazwa na kuchelewa kwa huduma ya maji kufika katika maeneo yao.


Amesema hali hiyo imekuwa ikiwasababishia wananchi gharama ya maisha, akieleza kuwa kipato cha baadhi yao kinategemea biashara ndogo ndogo ikiwemo kuuza mboga, samaki na shughuli nyingine za kujipatia kipato.


Mbunge Ngayiwa amesema suala hilo aliliwasilisha bungeni kwa waziri wa maji, na alichotarajia ni kukuta maji yakitoka, huku akitaka majibu ya wataalamu wa maji kuhusu adha hiyo kwa wananchi.



“Bungeni niliongea na nikambana Mhe waziri wa maji kwamba Lugela tenki linakamilika lini? Na akaniahidi linakamilika mapema kabla kabla ya mwaka huu kuisha.” Amesema Ngayiwa



“Tanki limekamilika, kazi iliyobaki ni kusambaza mabomba ili maji yaweze kufika katika makazi yetu. Nimepita huku na nimeona mabomba yanaendelea kulazwa,”


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nyahanga, Josephine Kilimba, amesema changamoto iliyopo sasa ni kuhakikisha mabomba yanafika katika maeneo yenye mahitaji makubwa ili wananchi wasilazimike kutumia gharama kubwa kuvuta maji kutoka maeneo ya mbali.


Amesema kukamilika kwa tenki ni hatua muhimu, lakini kazi inayofuata ni usambazaji wa mabomba, akisisitiza umuhimu wa kufanyika kwa survey ili kubaini maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo.


Naye Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA), John Mkama, amesema mabomba yaliyopo yanaendelea kusambazwa kulingana na upatikanaji wake, huku akieleza kuwa mitaro iliyowahi kuchimbwa na wananchi itatumika katika kukamilisha usambazaji wa maji.


Mkama amesema taratibu za upatikanaji wa mabomba mengine zinaendelea, ili kukamilisha maeneo yote yaliyokuwa yameandaliwa.


Amesema lengo la KUWASA ni kuyasogeza mabomba karibu na makazi ya wananchi ili kupunguza gharama za kuunganisha huduma ya maji, huku akieleza kuwa zoezi hilo linatarajiwa kuendelea kwa kipindi cha miezi kadhaa.


Akihitimisha, Ngayiwa amesisitiza kuwa baada ya kukamilika kwa tanki, hatua muhimu sasa ni kuhakikisha mabomba yanafika katika maeneo ya wananchi na huduma ya maji inapatikana kwa uhakika.


Amesema wananchi wanapaswa kuendelea kujiandaa kwa kuomba kuunganishiwa huduma, mara mabomba yanapofika katika maeneo yao.


Aidha amewataka KUWASA kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unafanyika kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi.






No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso