NGAYIWA AAHIDI KUENDELEA KUISEMEA KAGONGWA B, ATOA WITO KWA WAZAZI KUIMARISHA LISHE SHULENI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 18 September 2026

NGAYIWA AAHIDI KUENDELEA KUISEMEA KAGONGWA B, ATOA WITO KWA WAZAZI KUIMARISHA LISHE SHULENI

KAHAMA

Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, ameahidi kuendelea kuisemea Shule ya Msingi Kagongwa B ili pindi Serikali itakapoajiri walimu wapya, baadhi yao wapelekwe shuleni hapo kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu.

Ngayiwa ametoa ahadi hiyo wakati akishiriki mahafali ya sita ya Shule ya Msingi Kagongwa B, ambapo jumla ya wanafunzi 144, wakiwemo wasichana 88 na wavulana 56, walihitimu elimu ya msingi.

Shule hiyo kwa sasa ina jumla ya walimu 11 pamoja na walimu watatu wa kujitolea, hali ambayo imeendelea kuhitaji juhudi za pamoja kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia na walimu wa kutosha.

Akizungumzia suala la elimu, Mbunge Ngayiwa amewataka wadau wa elimu katika Wilaya ya Kahama, pamoja na wazazi, kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha lishe shuleni, akieleza kuwa upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi unaweza kuwasaidia kuzingatia zaidi masomo yao.


“Wilaya yetu, na hasa Manispaa yetu ya Kahama bado iko nyuma sana katika suala la lishe shuleni, Tunazidiwa na Ushetu na Msalala,” amesema Ngayiwa.

Aidha, Ngayiwa amewapongeza walimu wote katika Manispaa ya Kahama kwa kazi wanayoendelea kuifanya ya kuwaelimisha watoto, huku akitoa pongezi za pekee kwa walimu wa Shule ya Msingi Kagongwa B kutokana na matokeo mazuri ya mitihani ya darasa la saba.

Amesema Kagongwa B imekuwa ikiongoza kwa matokeo ya mtihani wa darasa la saba kiwilaya kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, akiwataka walimu kuendelea kulinda na kuboresha mafanikio hayo.

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo ameahidi kushughulikia baadhi ya changamoto zinazokabili shule hiyo, ikiwemo uhaba wa meza 10 za walimu, viti 10 pamoja na makabati mawili kwa ajili ya kutunzia nyaraka muhimu za shule.

Kwa upande wa wanafunzi waliohitimu, Ngayiwa amewasihi kuendelea kuthamini elimu na kuongeza bidii watakapojiunga na elimu ya sekondari, akiwataka kutokata tamaa katika safari yao ya kielimu.

Pia amewataka wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kujiunga na kidato cha kwanza na kuhakikisha hakuna mtoto hata mmoja anayekatishwa masomo kwa sababu yoyote ile.

Mbunge huyo pia alitoa wito kwa wazazi kuendelea kuwa karibu na watoto wao kwa kuwashauri kuhusu mienendo mizuri ya kitabia, pamoja na kudhibiti matumizi mabaya ya teknolojia na mitandao ya kijamii, ili kuwajenga kuwa vijana wenye maadili na kuwa hazina kwa Taifa na jamii kwa ujumla.






No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso