MWENGE WA UHURU WAPOKELEWA KAHAMA, MIRADI 21 YENYE THAMANI YA BILIONI 5.4 YAKAGULIWA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 21 August 2026

MWENGE WA UHURU WAPOKELEWA KAHAMA, MIRADI 21 YENYE THAMANI YA BILIONI 5.4 YAKAGULIWA



Na Neema Nkumbi, Kahama


Mwenge wa Uhuru umepokelewa katika Wilaya ya Kahama na kufanya ziara ya kukagua miradi 21 ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 5.4.


Katika ziara hiyo, Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika ujenzi wa madarasa matatu katika Shule ya Sekondari Kagongwa, mradi wenye thamani ya Shilingi milioni 70.4.


Kati ya fedha hizo, Shilingi milioni 63 zimetokana na mapato ya ndani ya Halmashauri, huku Shilingi milioni 7.4 zikiwa ni nguvu za wananchi.


Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Mkimbiza Mwenge Kitaifa, Wazo Michaelo, amesema mradi huo una ubora na unaendelea vizuri, huku kilichobaki kikiwa ni kukamilisha baadhi ya hatua za mwisho za ujenzi.


Aidha, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto shule na kufuatilia maendeleo yao ya kielimu, ikiwemo kujiridhisha kama watoto wao wanahudhuria masomo ipasavyo.


Amesisitiza pia umuhimu wa wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu, kuhifadhi mazingira na kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kwa ajili ya kujenga jamii yenye maendeleo endelevu.


Ziara ya Mwenge wa Uhuru inaendelea katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kahama kwa ajili ya kukagua na kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Ujumbe wa mwenge mwaka huu ni Amani, Umoja na Mshikamano Kitaifa.
" Tanzania ni yetu sote tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo".

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso