BULYANHULU YAELEZA TEKNOLOJIA ZA USALAMA, KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA BULYHULU KUZINGATIA USALAMA KAZINI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 23 September 2026

BULYANHULU YAELEZA TEKNOLOJIA ZA USALAMA, KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA BULYHULU KUZINGATIA USALAMA KAZINI

Mwenyekiti wa Kudumu wa Kamati ya Bunge Ustawi na Maendeleo ya Jamii , Hawa Mchafu Chakoma akisalimiana na Meneja Mahusiano ya Jamii na Mazingira wa Barrick Bulyanhulu , Agapiti Paul

Na Neema Nkumbi, Kahama

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imefanya ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, unaomilikiwa na kampuni ya Barrick, kujionea utekelezaji wa sheria za kazi na mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi, huku ikiibua maswali kuhusu ulinzi wa wafanyakazi, huduma kwa watu wenye ulemavu, wazee na mchango wa mgodi kwa jamii inayouzunguka.

Katika ziara hiyo iliyofanyika Septemba 23, 2026, wajumbe wa Kamati wamepokea maelezo kuhusu matumizi ya teknolojia katika kudhibiti vihatarishi vya uchimbaji, ukaguzi wa OSHA, ajira zinazotokana na shughuli za mgodi pamoja na miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR).

Akitoa taarifa kwa Kamati, Naibu waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano Eveline Munisi, amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali kwa kushirikiana na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ilifanya jumla ya kaguzi 871 katika Mkoa wa Shinyanga, huku wafanyakazi 7,969 wakipimwa afya zao.

Amesema katika kipindi hicho waajiri 102 walitekeleza matakwa ya sheria za usalama na afya mahali pa kazi na kupatiwa leseni za ithibati, huku waajiri wengine 83 wakipewa hati za maboresho ili kurekebisha maeneo yaliyobainika kuwa na changamoto.

Aidha, wafanyakazi 931 wa mgodi wa Bulyanhuli wamepatiwa mafunzo ya usalama na afya kazini.


TEKNOLOJIA YAPUNGUZA KUJIWEKA HATARINI

Akieleza hatua zinazochukuliwa na mgodi, meneja mahusiano na mazingira mgodi wa  wa Bulyanhulu Agapith Paul amesema kampuni imewekeza katika mifumo ya teknolojia na udhibiti wa kiutawala ili kupunguza uwezekano wa wafanyakazi kuathiriwa na vihatarishi vinavyotokana na shughuli za uchimbaji.

Amesema miongoni mwa hatua hizo ni matumizi ya mifumo ya automation inayowezesha baadhi ya shughuli za uchimbaji chini ya ardhi kufanywa na mashine zinazodhibitiwa na waendeshaji walioko juu ya ardhi.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, teknolojia hiyo hutumika katika maeneo hatarishi, ikiwemo shughuli za kuondoa vifusi baada ya milipuko, na kupunguza ulazima wa wafanyakazi kuingia katika maeneo yenye miamba inayoning’inia.

Mgodi pia umetumia mifumo ya kudhibiti uchovu kwa waendeshaji wa magari na mitambo, ambayo hutoa tahadhari operator anapoanza kupoteza umakini, huku taarifa zikifikishwa kwa wasimamizi kwa ajili ya hatua zaidi.

Aidha, baadhi ya magari na mitambo imewekewa mifumo inayotoa tahadhari dhidi ya matumizi ya simu wakati wa kuendesha, hatua inayolenga kupunguza usumbufu unaoweza kusababisha ajali.

Amesema kila mfanyakazi pia amepewa mamlaka ya kusimamisha kazi anapoona mazingira si salama kupitia utaratibu unaojulikana kama Stop Work Authority.

Katika mafunzo, wafanyakazi wapya na waendeshaji wa mitambo hupitia mafunzo ya nadharia, vitendo na mifumo ya majaribio (simulation) kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi katika mazingira halisi ya chini ya ardhi.

KAMATI YAIBUA HOJA ZA WATU WENYE ULEMAVU

Wakati wa majadiliano, mmoja wa wajumbe wa Kamati ambaye ni mbunge wa viti maalumu Mariamu Kisangi amehoji namna mgodi unavyohakikisha watu wenye ulemavu wanapata vifaa saidizi na kama miundombinu inayojengwa kupitia miradi ya CSR inazingatia mahitaji yao.

Mjumbe huyo pia alitaka kufahamu iwapo mgodi umekuwa ukishirikiana na watu wenye ulemavu katika kubaini mahitaji yao na kuhakikisha miundombinu inayojengwa inakuwa rafiki na inayofikika kwao.

Akijibu hoja hiyo, mwakilishi wa mgodi amesema kampuni hushirikisha wananchi, wakiwemo watu wenye ulemavu, katika kubaini mahitaji yao na kupanga miradi ya kuwasaidia.

Amesema mgodi hushirikiana na wataalamu wa Serikali, wakiwemo maafisa maendeleo ya jamii, katika kutambua vifaa saidizi vinavyohitajika na kuvifikisha kwa walengwa kupitia Serikali.

Kuhusu elimu, amesema mgodi umewekeza katika Shule ya Msingi Segese inayohudumia watoto wenye ulemavu, ikiwemo ujenzi wa uzio na mabweni kwa ajili ya wanafunzi hao.

WAZEE, CSR NA KITUO CHA UWEZESHAJI KAHAMA

Katika hoja nyingine, wajumbe walihoji namna mgodi unavyogawa miradi ya CSR katika maeneo yanayozunguka shughuli zake na kutaka makundi mbalimbali ya jamii, hususan wazee, yazingatiwe katika mipango ya maendeleo.

Mwakilishi wa mgodi amesema shughuli za CSR na huduma nyingine hutekelezwa kwa kuzingatia utaratibu wa mgawanyo ulioelekezwa na Serikali, ambapo asilimia 75 hutengwa kwa Halmashauri ya Msalala na asilimia 25 kwa Halmashauri ya Nyang’hwale.

Kuhusu wazee, amesema mgodi una mpango wa kuwapatia kadi za matibabu wazee wanaoishi katika Halmashauri ya Msalala, huku wale wanaohitaji huduma ambazo hazijajumuishwa katika mfumo wa NHIF wakisaidiwa na mgodi.

Ameongeza kuwa baadhi ya wazee wamewahi kusaidiwa kupata matibabu katika hospitali za rufaa, ikiwemo Hospitali ya Bugando.

Katika kikao hicho, Katibu tawala mkoa wa Shinyanga.. ameomba Barrick kuangalia uwezekano wa kusaidia ujenzi au urejeshwaji wa Kituo cha Uwezeshaji Wananchi cha Kahama, akieleza kuwa kituo hicho kilikuwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Katibu tawala  huyo amesema kituo hicho kilikuwa kikitoa huduma muhimu kwa wananchi wa Kahama na maeneo mengine ya Shinyanga, hivyo akaiomba kampuni kushirikiana na Serikali na wadau wengine kukisaidia.



Mgodi huo ulikaguliwa na OSHA Januari 2026 na kupatiwa ithibati Machi mwaka huo, baada ya maeneo yaliyohitaji maboresho kutambuliwa na kuanza kufanyiwa marekebisho.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama , Frank Nkinda ameshukuru Barrick Bulyanhulu kwa mahusiano mazuri kati yao na ofisi yake pia kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali za kuwaletea wananchi maendeleo na kushirikiana na vijiji 16 vinavyozunguka mgodi huo kwa kuwapatia wanawake , vijana na makundi mbalimbali katika jamii nafasi ya kufanya kazi na mgodi huo ili kujikwamua na  umasikini licha ya wengine kuwa na elimu ndogo.

Ziara hiyo imelenga kuipa Kamati nafasi ya kujionea utekelezaji wa sheria za kazi, mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi pamoja na namna shughuli za mgodi zinavyohusiana na ustawi wa wafanyakazi na jamii inayozunguka eneo la uchimbaji.

Mgodi wa Bulyanhulu umetoa ajira za moja kwa moja kwa wafanyakazi 1587.





No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso