Serikali inaandaa mpango wa matumizi ya maeneo ya maji ikiwa ni mkakati wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu kwa lengo la kuhakikisha sekta hiyo inakuwa endelevu na yenye kuleta manufaa makubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Mpango huo wa matumizi ya maeneo ya maji maarufu kama Marine Spatial Plan utasaidia kubainisha maeneo ya kimkakati yatakayochagiza shughuli mbalimbali zinazohusiana na uchumi wa buluu kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 na mkakati wake wa utekelezaji wa miaka kumi kuanzia mwaka 2024 hadi 2034.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mhe. Reuben Kwagilwa, alisisitiza kuwa serikali kupitia ofisi hiyo imejipanga kuimarisha shughuli za kiuchumi zinazotokana na rasilimali za maji.
Pamoja na hatua hizo, Mhe. Kwagilwa aliiarifu kamati hiyo kuwa Tanzania inaendelea na maandalizi ya Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 6 hadi 9, 2026, ambapo mkutano huo utawahusisha wadau mbalimbali pamoja na wabunge.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, aliishauri serikali kuwekeza nguvu katika kutoa elimu kwa wananchi ili watambue fursa pana zilizopo katika sekta hiyo, akibainisha kuwa wengi wanadhani uchumi wa buluu unahusu bahari pekee wakati unajumuisha maeneo mengine muhimu kama vile nishati, usafirishaji, utalii, madini, mazingira na viwanda.
Tangu kuanza kwa utekelezaji wa mkakati huo, serikali imefanikiwa kuimarisha uratibu na usimamizi wa rasilimali za bahari, mito, maziwa, maji ya chini ya ardhi na maeneo oevu, hatua ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

No comments:
Post a Comment