Na Neema Nkumbi, Ushetu – Kahama
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Ushetu, Wilaya ya Kahama, limejadili kwa kina hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo, huku madiwani wakieleza changamoto zinazohitaji hatua za haraka kutoka kwa mamlaka husika.
Katika kikao hicho, madiwani waliwasilisha hoja mbalimbali kwa Kaimu Meneja wa RUWASA Kahama, Rahel Antony Buliba, wakitaka ufafanuzi kuhusu maendeleo ya miradi ya maji, upanuzi wa mitandao, usimamizi wa vyanzo vya maji pamoja na namna ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma endelevu.
Diwani wa Kata ya Kisuke, Paul Golani, ameitaka RUWASA kuangalia uwezekano wa kupanua mitandao ya maji katika maeneo ambayo tayari yana vyanzo lakini wananchi bado hawajanufaika kikamilifu kutokana na uchache wa miundombinu ya usambazaji.
Amesema baadhi ya maeneo yana maji lakini changamoto kubwa ipo kwenye mtandao mdogo wa mabomba unaoshindwa kufikia makazi mengi ya wananchi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Chambo, Jumanne Gwessa, ameeleza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa vikundi vinavyosimamia miradi ya maji, akibainisha kuwa baadhi ya maeneo yanategemea chanzo kimoja cha maji hivyo yanahitaji usimamizi mzuri ili huduma isiathirike.
Naye Diwani wa Kata ya Kinamapula, Sharifu Samwel, amezungumzia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji, akitaka kuwepo kwa taarifa sahihi kuhusu hatua za miradi hiyo pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa maeneo yanayotarajiwa kunufaika.
Amesisitiza umuhimu wa RUWASA kushirikiana na viongozi wa kata na vijiji katika kutoa taarifa na elimu kuhusu miradi ya maji ili wananchi waweze kufahamu hatua mbalimbali za utekelezaji.
Diwani wa Kata ya Nyankende, Juba B. Juba, naye amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuboresha huduma ya maji na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa majibu kwa wakati.
Akijibu hoja hizo, Kaimu Meneja wa RUWASA Kahama, Rahel Antony Buliba, amewashukuru madiwani kwa ushirikiano na michango yao, akieleza kuwa taasisi hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Amesema utekelezaji wa miradi ya maji unahusisha hatua mbalimbali ikiwemo kazi za kiufundi na kijamii, huku akibainisha kuwa baadhi ya changamoto zinahitaji ushirikiano wa viongozi, wataalamu na wananchi ili kupata suluhisho la kudumu.
Ameeleza kuwa RUWASA inaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi na kuboresha huduma, pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu, Gagi Lala Gagi, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi, wataalamu na wananchi katika kutatua changamoto za huduma za maji.
Amesema changamoto zinazojitokeza zinapaswa kufanyiwa kazi kwa pamoja ili kuboresha huduma na kuhakikisha wananchi wanapata majibu ya hoja zao.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emanuel Cherehani, ameeleza umuhimu wa kutumia ipasavyo vyanzo vya maji vilivyopo, akitaka maeneo yenye miundombinu ya maji kuhakikisha wananchi wananufaika na uwekezaji huo.
Naye Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM Ushetu, Joachim Simbila, amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa haraka wa miradi ya maendeleo kwa ushirikiano wa viongozi na wataalamu.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Hadija Kabojela amesema amepokea hoja na ushauri uliotolewa na viongozi mbalimbali na kwamba atazifanyia kazi pia ametoa wito wa kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa kwa ufanisi na changamoto zinazowakabili wananchi wa Ushetu zinapatiwa ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment