Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’onda, amewataka wananchi wa Kijiji cha Sunga, Kata ya Uyogo Halmashauri ya Ushetu Wilaya ya Kahama, kutunza chanzo cha maji kilichojengwa katika eneo hilo ili kuhakikisha kinadumu na kuendelea kuwahudumia wananchi kwa muda mrefu.
Mwang’onda ametoa rai hiyo wakati akikagua mradi wa maji katika Kijiji cha Sunga, ambao unahusisha uchimbaji wa kisima kirefu, ujenzi wa mnara wa tanki pamoja na mtandao wa mabomba kwa ajili ya kuwapatia wananchi maji safi na salama.
Amesema kisima hicho kina urefu wa kina cha mita 40 na kwa sasa kina uwezo wa kuzalisha takribani lita 2,200 za maji kwa saa, hivyo amewataka wananchi na viongozi kuhakikisha eneo la chanzo linatunzwa ipasavyo.
Amesema utunzaji wa chanzo hicho unapaswa kwenda sambamba na upandaji wa miti rafiki kwa maji katika maeneo yanayozunguka kisima, akieleza kuwa kutokulinda vyanzo kunaweza kusababisha maji kupungua au chanzo kukauka.
“Tuendelee kupanda miti rafiki katika eneo hili ambayo inavuta na kutunza maji, Tukiacha hivi hivi, maji yanaweza kufuata mikondo mingine na mwisho wa siku kisima chetu kikakauka,” amesema Mwang’onda.
Aidha, amewataka wananchi kuwa mabalozi wazuri wa kutunza miundombinu ya maji na kushirikiana na viongozi wa vijiji, kata pamoja na RUWASA kuhakikisha chanzo hicho kinabaki salama kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Mwang’onda amesema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Amesema katika ziara zao za Mwenge wa Uhuru wamekuwa wakishuhudia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji katika maeneo tofauti nchini, jambo linaloonesha namna Serikali inavyotekeleza dhamira yake ya kumtua mama ndoo kichwani.
Mbunge wa jimbo la Ushetu Emanuel Cherehan ameeleza kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi ya maji inayotekelezwa kwa fedha zilizotolewa na Serikali chini ya program ya malipo kwa matokeo, huku pia kukiwa na mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria unaotekelezwa kwa ajili ya Manispaa ya Kahama.
Cherehani amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maji, wakisema wananchi wa Nsunga sasa wameanza kupata huduma ya maji safi na salama karibu na maeneo yao.
Akizungumza mradi huo, Meneja wa Ruwasa Magili Maduhu amesema ujenzi wake umehusisha kisima, tanki na mnara pamoja na mtandao wa mabomba, huku maji yakiwa tayari yameanza kutoka na kutumika na wananchi.
Mwang’onda pia amewataka wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu nchini, akisisitiza kuwa mazingira ya amani yanawezesha Serikali kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.
“Tuendelee kulinda amani na utulivu, Nchi yetu iendelee kubaki na utulivu ili Serikali iweze kuendelea kutuletea maendeleo makubwa zaidi ya haya ambayo tumekwisha kuyaona,” amesema.
Kwa upande wao, wananchi wa Nsunga, Tatu Mangelya ameeleza kuwa kabla ya kukamilika kwa mradi huo walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya maji, ikiwemo kuamka nyakati za usiku na kusafiri umbali mrefu kutafuta maji.
Ester Richard amesema walilazimika kununua ndoo moja ya maji kwa Shilingi 500, huku wengine wakitumia maji kutoka kwenye mito na visima visivyo salama.
“Zamani tulikuwa tunaamka usiku kwenda kutafuta maji na wakati mwingine tunarudi asubuhi tukiwa tumepata ndoo moja au mbili tu, Kwa sasa tunafurahia kupata maji safi na salama karibu na makazi yetu,” amesema Ester Richard.
Felister Maduka amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maji na kumuomba aendelee kuwaletea wananchi maendeleo.
Mradi huo unatarajiwa kunufaisha wananchi 1,092, huku ukiwa na gharama ya Shilingi 82,660,989.52.



No comments:
Post a Comment