kushoto ni Mhandisi wa Tarura Masola Juma, aliyevaa kanzu ni Diwani wa kata ya Malunga Ahmed Haruna, aliyevaa nguo nyeusi ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Masudi Kibetu na kulia aliyevaa shati la mikono mirefu na kofia ni Meya wa Manispaa ya Kahama Mataluma Kaniki
Na Neema Nkumbi, Kahama
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, kwa kushirikiana na Meya wa Manispaa hiyo, Mataluma Kaniki, Mhandisi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Masola Juma, pamoja na Diwani wa Kata ya Malunga Ahmed Haruna, wamefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya manispaa hiyo.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni ujenzi wa barabara ya maeneo ya viwanda vya kuchakata mpunga katika Kata ya Malunga, ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami kwa lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri na kuwezesha shughuli za uzalishaji na biashara kufanyika kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mhandisi wa TARURA, Masola Juma, amesema utekelezaji wa mradi huo unaendelea vizuri na mkandarasi anaendelea na kazi kwa mujibu wa mpango uliowekwa, Ameeleza kuwa ubora wa kazi unaendelea kufuatiliwa ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, amemtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha mradi ndani ya muda wa mkataba na kutoa taarifa mapema endapo kutajitokeza changamoto yoyote inayoweza kuathiri maendeleo ya kazi au shughuli za wananchi.
Naye Meya wa Manispaa ya Kahama, Mataluma Kaniki, amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi, akisisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti ili fedha zinazotolewa zitoe thamani iliyokusudiwa.
Diwani wa Kata ya Malunga Ahmed Haruna ameishukuru Serikali kwa kupeleka mradi huo katika kata yake, akisema utarahisisha usafirishaji wa mazao ya mpunga, kuongeza fursa za kiuchumi na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika eneo la viwanda vya kuchakata mpunga.
Mbali na ukaguzi wa barabara hiyo, viongozi hao walitembelea pia eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa mashine za kuchakata mpunga lililopo kata ya Busoka na kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa eneo, wananchi na taasisi zinazohusika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Pia wametembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya uchenjuaji madini lililopo Nyashimbi kata ya mhongolo ambapo waliambatana na diwani wa kata hiyo Mariamu Galula na diwani wa kinaga Gerald Joseph, Afisa madini kahama, Meneja wa Kuwasa, Mhandisi wa Tanesco na wazee wa eneo hilo.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Manispaa ya Kahama kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inasimamiwa kwa karibu ili ikamilike kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.












No comments:
Post a Comment