
Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, akizungumza na wananchi wa kata ya Mhungula juu ya umaliziaji wa boma la za zahanati
Muonekano wa jengo la zahanati ya Mhukgula mara baada ya kupauliwa
Na Neema Nkumbi, Kahama
Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, amefanikisha uwekaji wa paa katika jengo la Zahanati ya Mtaa wa Mhungula, Kata ya Mhungula, Manispaa ya Kahama, baada ya kutumia Shilingi milioni 30 kutoka Mfuko wa Jimbo kukamilisha hatua hiyo.
Jengo hilo lilianza kujengwa mwaka 2010 kwa nguvu za wananchi, lakini lilikwama kwa kipindi cha takribani miaka 15 bila kukamilika, hali iliyosababisha wananchi wa eneo hilo kuendelea kutafuta huduma za afya katika maeneo ya mbali ikiwemo Kituo cha Afya Nyasubi na Hospitali ya Wilaya ya Kahama.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Mhungula, Mbunge Ngayiwa amesema kukamilika kwa uwekaji wa paa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi pamoja na ahadi alizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Amesema ataendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama kuhakikisha hatua zinazofuata zinafanyika ili zahanati hiyo ikamilike na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
“Lengo ni kuhakikisha wananchi wa Mhungula wanapata huduma za afya karibu na maeneo yao na kuondokana na changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu,” amesema Ngayiwa.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mhungula, Elisha William Lutubija, amesema ndani ya kipindi cha miezi saba tangu uchaguzi uliofanyika mwaka 2025, Serikali imetoa zaidi ya Shilingi milioni 500 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata hiyo.
Mkazi wa Mhungula, Salma Nati, amempongeza Mbunge Ngayiwa kwa kuanza kutekeleza ahadi zake na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi.
Naye Katani Zonzo ameomba Serikali kuongeza juhudi za kukamilisha zahanati hiyo, akieleza kuwa jengo hilo kwa muda mrefu limekuwa halitumiki na baadhi ya wahalifu kulitumia kama sehemu ya kujificha nyakati za usiku.




No comments:
Post a Comment