Diwani wa Kata ya Mhongolo, Mariam Galula, akiungumza na wananchi wa mtaa wa Nyashimbi kata ya Mhongolo Manispaa ya Kahama
Afisa Mtendaji wa Kata ya Mhongolo akiungumza na wananchi wa mtaa wa Nyashimbi kata ya Mhongolo Manispaa ya Kahama
Na Neema Nkumbi Kahama
Wananchi wa Mtaa wa Nyashimbi, Kata ya Mhongolo katika Manispaa ya Kahama, wameiomba Serikali kuingilia kati changamoto ya uuzwaji holela wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya barabara, wakisema hali hiyo imewasababishia kukosa njia za kupita na kuathiri upatikanaji wa huduma muhimu.
Malalamiko hayo yametolewa katika mkutano wa Diwani wa Kata ya Mhongolo, Mariam Galula, na wananchi wa mtaa huo, ambapo baadhi yao wamedai kuwa maeneo yaliyokuwa yamepangwa kwa ajili ya barabara yamekuwa yakivamiwa na kuuzwa kwa watu binafsi.
Mkazi wa Nyashimbi, Jenipha Mwendo, amesema baadhi ya wananchi wamejikuta wakikosa hata njia za kupita kutokana na maeneo yanayopaswa kuwa barabara kuchukuliwa na watu wanaodaiwa kujihusisha na udalali wa ardhi.
“Kwetu hatuna barabara. Wanajua kabisa kuna barabara, lakini mtu anafika anasema kiwanja kimeuzwa. Hakuna barabara, hakuna hata pa kupita. Kwa nini tunafanyiwa hivyo?” amesema.
Amesema changamoto hiyo imekuwa kubwa zaidi katika maeneo ya chini ya Kanisa la Anglikana, ambako wananchi wanadai kukosa njia nzuri ya kupita, hali ambayo inaweza kuwa hatari wakati wa dharura kama wagonjwa wanapohitaji kusafirishwa.
“Hatuna hata pa kupita. Dalali anafika, anakamata eneo na kuuza, anayenunua anajenga kwa sababu ameandikiwa na mihuri imepigwa. Tukipata hata ugonjwa, hatuna pa kupita,” amesema.
Kwa upande wake, mkazi mwingine wa Mhongolo, Michael Philbetty, amesema viongozi wanapaswa kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto za barabara badala ya kuzikwangua na kuziacha bila hatua nyingine za uboreshaji.
Amesema kukwangua barabara bila kuweka kifusi au tabaka la kuimarisha barabara kunaweza kuongeza uharibifu hasa kipindi cha mvua.
“Kukwangua barabara na kuiacha hivi hivyo siyo kutengeneza bali ni kuongeza tatizo. Tunapoikwangua tunaacha ule udongo hauna chochote, mvua zinanyesha zinasomba zaidi,” amesema.
Philbetty amesema changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa Kata ya Mhongolo ni pamoja na barabara, umeme na maji, akitaka hoja zinazotolewa na wananchi zifanyiwe kazi kwa wakati.
“Jambo kubwa sana hapa ni barabara, umeme na maji. Tusichukue hoja na kuziweka kwenye mafaili, tuzishughulikie kwa sababu utekelezaji wa changamoto ndogo ndogo kwa wakati unaweza kusaidia kupunguza malalamiko ya wananchi,” amesema.
MGOGORO WA ARDHI WAIBUKA
Katika mkutano huo, mkazi mwingine wa Mtaa wa Nyashimbi ameibua changamoto ya ardhi akidai eneo lake liliwahi kuhusishwa na uuzwaji wa kiwanja bila yeye kufahamu, hali iliyosababisha mazao yake ya mihogo kung’olewa na baadaye msingi kujengwa.
Mkazi huyo amesema aligundua mihogo yake imeondolewa siku akiwa kanisani, na baada ya kufuatilia kwa majirani hakufanikiwa kumtambua mtu aliyehusika.
“Kwenye eneo langu kuna mtu aliwahi kuuziwa kiwanja siku ya Sabato nikiwa kanisani. Nilikuwa nimepanda mihogo, nikakuta mihogo imeng’olewa. Nikatoa taarifa kwa uongozi uliokuwepo enzi hizo,” amesema.
Amesema baadaye alikuta msingi umejengwa katika eneo hilo na licha ya kutoa taarifa kwa viongozi wa wakati huo, suala hilo limeendelea kwa miaka kadhaa bila kupata suluhisho.
Ameongeza kuwa msingi huo bado upo bila kuendelezwa na ameeleza kuwa anatarajia kuchukua hatua iwapo hakutakuwa na suluhisho la kudumu.
DIWANI AAHIDI KUFIKISHA HOJA ZA WANANCHI
Diwani wa Kata ya Mhongolo, Mariam Galula, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na viongozi katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili, akisema maendeleo ya kata hiyo ni jukumu la pamoja.
Galula amesema changamoto zote zilizowasilishwa na wananchi amezibeba na zitapelekwa katika maeneo husika kwa ajili ya kupatiwa majibu na hatua zaidi.
“Nyashimbi ni kweli kuna changamoto nyingi sana. Zote nimezibeba ambazo nimezijibu hapa, lakini zingine ambazo zinatakiwa kufika sehemu fulani nimezibeba na nitazifikisha,” amesema.
Amesema baadhi ya hoja zimeweza kujibiwa moja kwa moja katika mkutano huo, huku nyingine zikihitaji ushirikishwaji wa wataalamu na mamlaka husika.
Diwani huyo amewataka wananchi kuendelea kushiriki katika mikutano ya kijamii na kutoa maoni yao, akisisitiza kuwa maendeleo ya Nyashimbi yanahitaji ushirikiano kati ya wananchi na viongozi.
“Mimi peke yangu siwezi. Ninaweza tukishirikiana na ninyi ili kufikisha sehemu fulani. Nyashimbi ni kwetu, kwangu, kwenu, ni kwetu wote,” amesema.









No comments:
Post a Comment