Na Neema Nkumbi, Kahama
Halmashauri ya Manispaa ya Kahama imefanikiwa kusajili jumla ya vikundi 326 vya makundi maalum katika Mfumo wa Manunuzi ya Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST), sawa na asilimia 217 ya lengo lililowekwa, huku ikifanikiwa pia kutoa zabuni kwa vikundi hivyo.
Mafanikio hayo yameifanya Halmashauri ya Manispaa ya Kahama kutunukiwa tuzo na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kuonesha ufanisi mkubwa katika zoezi la kusajili na kutoa kazi (tender) kwa makundi maalum kupitia mfumo wa NeST.
Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Ndg. Masudi Kibetu, na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’onda, ikiwa ni sehemu ya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Serikali katika ziara ya Mwenge huo.
Halmashauri ya Manispaa ya Kahama ilikuwa imepewa lengo la kusajili vikundi 150 vya makundi maalum katika mfumo wa NeST, lakini imevuka lengo hilo baada ya kusajili vikundi 326, sawa na asilimia 217.
Kati ya vikundi hivyo, 173 ni vya vijana, 150 vya wanawake, viwili vya watu wenye ulemavu na kikundi kimoja cha wazee.
Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Bw. Mbwana Karata, amesema Halmashauri hiyo imetenga jumla ya Shilingi 1,943,353,500, sawa na asilimia 30 ya manunuzi ya Serikali, kwa ajili ya kuwawezesha makundi maalum kunufaika na fursa za zabuni.
Amesema hadi sasa, jumla ya vikundi vinne vimetunukiwa zabuni zenye thamani ya Shilingi 242,450,000.
Kati ya zabuni hizo, vikundi viwili vya vijana vimetunukiwa zabuni zenye thamani ya Shilingi 74,450,000, huku vikundi viwili vya wanawake vikipata zabuni zenye thamani ya Shilingi 168,000,000.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha makundi maalum yanapata fursa za kushiriki katika shughuli za kiuchumi kupitia mfumo wa manunuzi ya umma, pamoja na kuwawezesha vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na wazee kunufaika na fursa zinazotokana na matumizi ya fedha za Serikali.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Ndg. Masudi Kibetu, amesema tuzo hiyo si mafanikio yake binafsi, bali ni matokeo ya umoja, ushirikiano na juhudi za watumishi pamoja na viongozi wa Manispaa na Wilaya ya Kahama.
Amesema kutambuliwa na PPRA kupitia tuzo hiyo ni ishara kwamba ushirikiano uliopo katika utekelezaji wa majukumu ya Halmashauri umezaa matokeo chanya, huku akiwapongeza watumishi na viongozi wote walioshiriki katika kufanikisha zoezi hilo.
Mafanikio hayo yamepatikana katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya mfumo wa NeST katika ununuzi wa umma, kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na ushiriki wa makundi mbalimbali katika fursa za zabuni za Serikali.


















No comments:
Post a Comment