Na Neema Nkumbi, Kahama
Mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda ameupokea mwenge wa uhuru leo agosti 21, 2026 kutoka wa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro.
Mwenge wa Uhuru umezindua jengo maalumu la kuhudumia waraibu wa dawa za kulevya lililopo katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, lililogharimu zaidi ya Shilingi milioni 467.
Jengo hilo limejengwa kwa ufadhili wa Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, ambapo ujenzi wake ulianza Mei 11, 2025 na kukamilika Mei 11, 2026.
Akizungumza baada ya jengo hilo kuzinduliwa, mmoja wa waraibu wanaopatiwa huduma katika kituo hicho, Molitazi Maganga, amewashukuru Jeshi la Polisi pamoja na taasisi zinazopambana na dawa za kulevya kwa juhudi zao za kupunguza tatizo hilo nchini.
Maganga ameiomba Serikali na taasisi husika kuendelea kuziba mianya ya dawa za kulevya, ikiwemo kudhibiti uzalishaji na usambazaji wake, ili kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa janga hilo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, amesema kupambana na dawa za kulevya pekee haitoshi, bali ni muhimu pia kuweka mazingira mazuri kwa waraibu wanaopatiwa matibabu ili waweze kujishughulisha na shughuli za uzalishaji na kuongeza kipato.
Amesema kuwa waraibu wanapomaliza matibabu wanapaswa kupewa fursa na mazingira yatakayowasaidia kurejea katika maisha ya kawaida na kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Christina Mzava, amesema waraibu wanaopatiwa matibabu hawapaswi kuachwa baada ya kumaliza matibabu, bali wanahitaji kuendelea kusaidiwa hadi pale watakapoweza kujitegemea kiuchumi.
Mzava ameahidi kuwa mlezi wa waraibu hao, akisisitiza umuhimu wa kuwawezesha ili wasirudi katika matumizi ya dawa za kulevya kutokana na changamoto za kiuchumi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael, amesema ujenzi wa majengo kama hayo ulikuwa ukipatikana zaidi katika ngazi za mikoa, lakini sasa huduma hizo zimeanza kusogezwa hadi katika halmashauri.
Ameipongeza Manispaa ya Kahama kwa hatua hiyo na kuwataka wahusika kuhakikisha jengo hilo linatumika ipasavyo katika kuwahudumia vijana walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha, Wazo ameshauri waraibu waliopatiwa matibabu kuwezeshwa kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, ili waweze kuanzisha shughuli za uzalishaji na kujikwamua kiuchumi.
Amesema kuwa kuwawezesha kiuchumi ni sehemu muhimu ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kwa kuwa kutawasaidia kujitegemea na kupunguza uwezekano wa kurejea katika matumizi ya dawa hizo.
Mwenge wa Uhuru umelipongeza Manispaa ya Kahama kwa kutekeleza mradi huo na hatimaye kuzindua jengo hilo ambalo linatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma kwa watu wanaopambana na utegemezi wa dawa za kulevya.
No comments:
Post a Comment