WAISLAMU MASJID RAHMAN MONGOLO WAADHIMISHA MIAKA MITANO YA JUVIKIBA KWA KUCHANGIA DAMU SALAMA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 6 July 2026

WAISLAMU MASJID RAHMAN MONGOLO WAADHIMISHA MIAKA MITANO YA JUVIKIBA KWA KUCHANGIA DAMU SALAMA


Na Neema Nkumbi, Kahama

Wanachama wa Jumuiya ya Vijana wa Kiislamu (JUVIKIBA) ya Masjid Rahman iliyopo Kata ya Mongolo, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wameadhimisha miaka mitano tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii zikiwemo kutembelea wagonjwa, kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kushiriki zoezi la kuchangia damu salama ili kuokoa maisha ya wahitaji.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo, Mwenyekiti Mstaafu wa JUVIKIBA, Ibeshi Alphan Ibeshi, amesema jumuiya hiyo iliyoanzishwa Julai 4, 2021 imeamua kuadhimisha miaka yake mitano kwa vitendo vinavyoonyesha upendo na kuwajibika kwa jamii badala ya kufanya sherehe pekee.

Amesema baada ya kutembelea wagonjwa na watoto wanaohitaji msaada, wanachama walishiriki zoezi la kuchangia damu salama kwa lengo la kusaidia wanawake wanaojifungua, waathirika wa ajali pamoja na wagonjwa wengine wanaohitaji huduma hiyo muhimu hospitalini.

"Ni wajibu wetu kurejesha kwa jamii kile tunachoweza. Tunataka vijana watambue kuwa kuchangia damu ni kitendo cha kuokoa maisha ya watu wengine na ni sehemu ya kujenga jamii yenye mshikamano," amesema Ibeshi.

Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa zoezi hilo, Zuriet Ahmed , anesema amejitokeza kwa hiari kuchangia damu kwa kuwa anatambua umuhimu wake kwa wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu, huku akiwahimiza wananchi wengine kujitokeza kwa moyo wa kujitolea kila wanapopata fursa.

Naye Saidi Katala amesema maadhimisho hayo yamekuwa fursa ya kuwakumbusha vijana umuhimu wa kuwajibika kwa jamii kupitia matendo ya kujitolea, akibainisha kuwa mahitaji ya damu ni makubwa kutokana na ongezeko la ajali na changamoto zinazowakabili wanawake wajawazito wakati wa kujifungua.

Katala pia ametoa wito kwa waandaaji wa matukio mbalimbali kama bonanza na mikusanyiko ya kijamii kushirikiana na timu za damu salama ili kuwezesha wananchi wengi zaidi kuchangia damu na kuongeza akiba katika benki za damu.

Akizungumzia suala la amani, amesema mazingira ya utulivu ndiyo yanayowezesha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo na huduma za kijamii, hivyo akawahimiza wananchi wa Kahama na Watanzania kwa ujumla kuendelea kulinda amani kama msingi wa maendeleo.

Imamu wa Masjid Rahman Mongolo, Suleiman Kapesuke, amewapongeza vijana wa JUVIKIBA kwa kuandaa maadhimisho yenye manufaa kwa jamii, akisema kuchangia damu ni ibada ya kusaidia kuokoa maisha ya binadamu bila kujali dini, kabila au tofauti nyinginezo. Pia aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika kulinda amani, hususan kuelekea maadhimisho ya sikukuu za Sabasaba na shughuli nyingine za kitaifa.

Kaimu Mratibu wa Damu Salama Wilaya ya Kahama, Elibahati Mollel, amesema zoezi hilo limefanikiwa kupata wachangiaji zaidi ya 20 na kukusanya unit 21 za damu, akieleza kuwa ni mchango muhimu kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo hospitalini.

Amesema matumizi ya damu katika hospitali za wilaya ni makubwa kutokana na ajali za barabarani, huduma za wajawazito na wagonjwa wengine, hivyo akatoa wito kwa taasisi za dini, vikundi vya kijamii, waandaaji wa bonanza na wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana na timu ya damu salama ili kuongeza idadi ya wachangiaji na kuhakikisha benki ya damu inakuwa na akiba ya kutosha wakati wote.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso