Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ameagiza halmashauri zote sita za mkoa huo kutopokea dawa za matumizi ya binadamu zenye muda wa matumizi uliobaki chini ya miezi 12, akisema hatua hiyo inalenga kulinda fedha za umma na kuhakikisha wananchi wanapata dawa salama na zenye ubora.
Mhita ametoa agizo hilo wakati wa Baraza Maalum la kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama, baada ya kujitokeza hoja kuhusu dawa zilizonunuliwa zikiwa na muda mfupi wa matumizi.
Amesema halmashauri hununua dawa kwa ajili ya matumizi ya miezi sita hadi minane, hivyo si sahihi kupokea dawa ambazo zinaweza kuisha muda wake wa matumizi ndani ya miezi michache baada ya kupokelewa.
"Ndani ya Mkoa wa Shinyanga hatutakubali kabisa kuletewa dawa kwa ajili ya matumizi ya binadamu ambazo zimebakiza muda wa chini ya miezi 12," amesema Mhita.
Ameongeza kuwa dawa zinaposambazwa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati kisha kuisha muda wake wa matumizi, wananchi huanza kuilaumu Serikali wakidhani dawa zimefichwa, ilhali tayari zilikuwa zimefikishwa kwenye vituo vya kutolea huduma.
Mhita amesema iwapo dawa zinazohitajika hazipatikani, ni afadhali mamlaka husika zieleze hali halisi kuliko kupeleka dawa zinazokaribia kuisha muda wake wa matumizi na kusababisha hasara kwa Serikali.
Aidha, amewataka viongozi wa sekta ya afya kuimarisha ukaguzi wa dawa zinazoingia katika maghala na vituo vya kutolea huduma ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya muda wa matumizi kabla ya kupokelewa.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa agizo hilo utasaidia kuondoa upotevu wa fedha za umma, kuimarisha usimamizi wa dawa na kuongeza imani ya wananchi katika huduma za afya zinazotolewa na Serikali.
Awali akiwasilisha taarifa ya hoja za CAG, majibu ya menejimenti na hali ya utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Kaimu Mweka Hazina wa Halmashauri ya Ushetu, Charles Machuba, amesema mkaguzi alipendekeza menejimenti kuweka utaratibu wa kutambua na kuondoa kwa wakati dawa zinazokaribia kuisha muda wa matumizi, pamoja na kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinavyonunuliwa vinakuwa na muda wa matumizi usiopungua miezi 12.
Machuba amesema uongozi wa halmashauri uliwasilisha ombi Wizara ya Fedha la kufanyika ukaguzi wa suala hilo, ambapo Katibu Mkuu wa wizara hiyo alitoa mrejesho na wataalamu walifika kufanya ukaguzi kuanzia Aprili 19 hadi 21, 2026.
Ameeleza kuwa kwa sasa halmashauri inasubiri taarifa rasmi ya ukaguzi huo ili hatua zinazostahili ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa mapendekezo yaliyotolewa.
Kwa mujibu wa Machuba, CAG ametambua majibu yaliyowasilishwa na uongozi wa halmashauri, lakini akabainisha kuwa utekelezaji kamili wa mapendekezo hayo bado unasubiriwa.
Aidha, amesema Kamati ya Ukaguzi ilipendekeza kuundwa kwa kamati maalumu za ukaguzi wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuhakikisha zinapokelewa dawa zenye muda wa matumizi usiopungua miezi 12.





No comments:
Post a Comment