“Kwa hiyo ninawahimiza wafanyabiashara wa Ufaransa mtumie vyema fursa hii ya kipekee. Maamuzi yatakayofanywa leo ndiyo yatakayoamua mwelekeo wa sekta za uchumi za kesho kwa nchi zetu.
Dkt. Mwigulu amesema Ufaransa inao utaalamu wa hali ya juu na wa kiwango cha kimataifa katika teknolojia, uhandisi, nishati, miundombinu, viwanda, masuala ya fedha, na huduma za afya.
Amesema maeneo hayo yana nguvu na yanakamilishana kwani katika umoja wake yanajenga fursa za kipekee za kukuza maendeleo endelevu na ustawi wenye manufaa ya pande zote mbili.
“Tunapoanza kwa ujasiri kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Serikali yetu itaendelea kuwa thabiti katika kuhakikisha kunakuwepo mazingira yanayotabirika, yenye uwazi na rafiki kwa biashara, ambapo uwekezaji unalindwa, ushirikiano unathaminiwa, na mafanikio yanawanufaisha wadau wote,” amesisitiza.
Waziri Mkuu pia alishuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Chama cha Kimataifa cha Biashara cha Ufanransa (ICC) na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), ambapo Mtendaji Mkuu wa TPSF, Bw. Deo Massawe alibadilishana hati hiyo na Naibu Katibu Mkuu wa ICC, Bw. Julian Kassum.
Mapema, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, aliwaeleza washiriki wa mjadala huo kwamba kitendo kilichofanyika leo kinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo inasisitiza ushiriki wa sekta binafsi kwa asilimia 70 katika kuchochea maendeleo ya uchumi.
Kwa upande wake, Rais wa TPSF, Bi. Angelina Ngalula alisema Tanzania ipo katika nafasi ya kipekee ya kuwa kitovu cha mageuzi ya uchumi barani Afrika chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Kwa miaka mingi, Ufaransa imekuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika uwekezaji. Hata hivyo, kwa sasa tunapaswa kuelekeza nguvu zetu katika kujenga ushirikiano wa muda mrefu utakaokuza uhamishaji wa teknolojia, kukuza sekta ya utalii, huduma za kifedha pamoja na uchumi wa kidijitali. TPSF iko tayari kuwezesha ushirikiano huo kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao wa Ufaransa,” alisema.
Baadhi ya kampuni za Ufaransa zilizoshiriki mjadala huo zinajihusisha na usimamizi wa nishati ya jua (ikiwemo mifumo ya taa za barabarani), usafirishaji, maji, nishati, ujenzi, viwanda, mazingira na ufugaji wa viumbe maji (ikiwemo uzalishaji wa mwani wa baharini).
Kampuni nyingine ni waendeshaji wa huduma za satelaiti wanaotoa suluhisho bunifu kwa huduma za utangazaji wa sauti na picha, intaneti ya kasi (broadband), huduma za data, usafiri wa baharini na anga. Aidha, kulikuwa na wazalishaji wa mabomba maalumu yanayotumika katika sekta ya mafuta na gesi.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde; Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi; Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UNESCO, Balozi Saidi Othman Yakubu; Mtendaji Mkuu wa MEDEF International, Bw. Philippe Gautier; Rais wa Baraza la Biashara la Ufaransa na Afrika Mashariki, Bi. Celine Gouveia; pamoja na wajumbe kutoka sekta binafsi ya Tanzania na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Ufaransa.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JULAI 6, 2026.
No comments:
Post a Comment