Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kikodi Kahama, Leonard Kamwamu akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Na Neema Nkumbi, Kahama
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kikodi Kahama, Leonard Kamwamu, amesema ushirikiano wa ndani ya taasisi, viongozi wa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na utoaji wa elimu kwa walipakodi, ni miongoni mwa sababu zilizochangia mafanikio ya ukusanyaji wa mapato katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Kamwamu amesema katika mwaka huo TRA Mkoa wa Kikodi Kahama ilikuwa na lengo la kukusanya zaidi ya Sh. bilioni 35 lakini wameweza kukusanya zaidi ya bilioni 47 na kufanikiwa kuvuka lengo hilo kwa kufikia zaidi ya asilimia 132 ya makusanyo yaliyokusudiwa.
"Mafanikio haya yametokana na ushirikiano mkubwa ndani ya ofisi kati yangu, wasaidizi wangu na wafanyakazi wote, Pia tumepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama ambao wamekuwa mstari wa mbele kutusaidia kila tulipohitaji," amesema Kamwamu.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2026/2027, TRA imeongezewa lengo la ukusanyaji wa mapato mpaka kufikia bilioni 50.4 na kwamba itaendelea kutumia njia ya mazungumzo na walipakodi badala ya migogoro ili kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake wa kulipa kodi.
Hata hivyo, ametaja changamoto zinazoendelea kujitokeza kuwa ni baadhi ya wafanyabiashara kushindwa kutoa risiti za kielektroniki na kuchelewa kuwasilisha taarifa za mapato (returns), hali inayodhoofisha ufanisi wa ukusanyaji wa kodi.
Kamwamu amesema TRA itaongeza usimamizi katika sekta ya madini, ubia wa biashara (joint ventures) na taasisi za elimu binafsi ili kuhakikisha shughuli zote zinazostahili kulipa kodi zinafanya hivyo kwa mujibu wa sheria.
"Hatutaki kuwa na uadui na walipakodi, Tunataka TRA ionekane kama taasisi rafiki, Dhamira yetu ni kuwa na 'kodi za tabasamu', ambapo mlipakodi anapata huduma bora na anatimiza wajibu wake kwa hiari," amesema.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Kahama, Charles Machali, amesema maboresho ya mifumo ya TRA yamepunguza urasimu na kuimarisha mahusiano kati ya mamlaka hiyo na wafanyabiashara.
"Siku hizi ukifika TRA unasikilizwa na unapatiwa suluhisho, Hofu iliyokuwepo zamani imepungua, ndiyo maana tunawaomba waendelee kutoa elimu kwa wafanyabiashara," amesema.
Naye mfanyabiashara wa samani, Bondes Pantaleon, amesema huduma za elimu kwa walipakodi ikiwemo ofisi inayotembea (mobile office) zimekuwa msaada mkubwa kwa wafanyabiashara kwa kuwa zinawafikia moja kwa moja katika maeneo yao ya biashara na kuwajengea uelewa wa masuala ya kodi.
Amesema hatua hiyo imeimarisha ushirikiano kati ya TRA na wafanyabiashara na kuchochea mazingira bora ya biashara katika Manispaa ya Kahama.


No comments:
Post a Comment