MBUNGE NGAYIWA ARIDHISHWA NA UJENZI WA JENGO LA MAMA NA MTOTO, AAHIDI KUFUATILIA GHARAMA ZA UMEME KATIKA JENGO LA UZALISHAJI OXYGEN HOSPITALI YA MANISPAA YA KAHAMA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 24 July 2026

MBUNGE NGAYIWA ARIDHISHWA NA UJENZI WA JENGO LA MAMA NA MTOTO, AAHIDI KUFUATILIA GHARAMA ZA UMEME KATIKA JENGO LA UZALISHAJI OXYGEN HOSPITALI YA MANISPAA YA KAHAMA

 

Kushoto ni Mganga mfawidhi wa hospitali ya Manispaa ya  Kahama Dkt Michael Mushi, katikati ni Mbunge wa jimbo la Kahama mjini Benjamin Ngayiwa akizungumza baada ya kutembelea na kuona uboreshaji wa hospitali hiyo na kulia ni Mganga mkuu wa Hospitali ya wilaya ya Kahama Dkt Baraka Msumi.

Hili ni dilisha linalompa fursa mwananchi kuuliza kushauri kutoa maoni au malalamiko yoyote kuhusu huduma zinazopatikana katika hospitali ya manispaa ya Kahama

Na Neema Nkumbi, Kahama

Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, ambalo limefikia asilimia 85 ya utekelezaji, akisema mradi huo utakuwa hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya na kupunguza vifo vya akina mama wajawazito pamoja na watoto wachanga.

Mbunge huyo ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea hospitali hiyo na kufanya mazungumzo na viongozi wa afya, akiwemo Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kahama, Dkt. Baraka Msumi, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Dkt. Michael John Mushi, pamoja na Muuguzi Mfawidhi, Magreth Kienzi, kabla ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa.

"Nimefurahishwa na kazi ya umaliziaji wa jengo la Mama na Mtoto, Tumezunguka na kujionea jinsi lilivyojengwa vizuri Jengo hili litasaidia kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga Pia nimeona ujenzi wa jengo la huduma za bima unaendelea na maandalizi ya ujenzi wa kitengo cha huduma za dharura (Emergency Department), jambo ambalo ni maendeleo makubwa kwa Manispaa yetu ya Kahama," amesema Ngayiwa.

Mbunge huyo amewataka viongozi wa sekta ya afya kuendelea kusimamia ubora wa huduma kwa wananchi huku wakishughulikia malalamiko yanayowasilishwa na wananchi, akibainisha kuwa ongezeko la wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Nyasubi linahitaji mipango ya kuboresha huduma ili kuepusha msongamano.

Kuhusu changamoto ya gharama kubwa za umeme zinazotumika kuendesha mtambo wa kuzalisha hewa tiba (Oxygen Plant), Ngayiwa amesema atafanya mazungumzo na Meneja wa TANESCO pamoja na Waziri wa Nishati ili kutafuta suluhisho litakalopunguza gharama hizo.

"Tutaongea na Meneja wa TANESCO pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Nishati kuona kama kuna uwezekano wa kupunguza gharama za uwezo wa umeme ili hospitali ibaki kulipia matumizi halisi ya umeme, Hilo litasaidia kupunguza gharama za uzalishaji wa oxygen na kuongeza uwezo wa hospitali kuendelea kutoa huduma muhimu kwa wananchi," amesema.

Aidha, amewataka viongozi wa hospitali kuanzisha utaratibu wa kuwatambua na kuwapongeza watumishi wanaofanya vizuri, akiahidi kushirikiana nao kutafuta namna ya kuwazawadia ili kuongeza ari ya utendaji.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kahama, Dkt. Baraka Msumi, amesema ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto ni sehemu ya mpango mpana wa kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo.

Amesema hospitali tayari imekamilisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) pamoja na jengo la uchunguzi, ambayo yote yanaendelea kutoa huduma, huku jengo la Mama na Mtoto likitarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba mwaka huu.

"Jengo la Mama na Mtoto limefikia asilimia 85 ya utekelezaji na linajengwa na mkandarasi SUMA JKT kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 6.1, Pia tunaendelea na ujenzi wa jengo la huduma za bima ambalo litaboresha utoaji wa huduma kwa wanachama wa mifuko mbalimbali ya bima za afya," amesema Dkt. Msumi.

Ameongeza kuwa jengo la huduma za bima litakuwa na madaktari, maabara, famasi na huduma nyingine zote muhimu katika eneo moja, hatua itakayopunguza msongamano na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Dkt. Michael John Mushi, amesema pamoja na maboresho ya miundombinu, hospitali inakabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za umeme kwa ajili ya kuendesha mtambo wa kuzalisha hewa tiba.

Amesema mfumo wa malipo wa postpaid unaifanya hospitali kulipa gharama za matumizi ya umeme pamoja na gharama za uwezo wa umeme (KVA), hali inayoongeza mzigo mkubwa wa uendeshaji.

"Tumeiandikia TANESCO tukieleza changamoto hii ili tupate ushauri na msaada. Hewa tiba ni huduma muhimu kwa kina mama wajawazito, wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji na watoto wachanga, ambao wengi wao hupata huduma bila malipo kwa mujibu wa sera ya Serikali. Kupungua kwa gharama za umeme kutasaidia huduma hii kuwa endelevu," amesema Dkt. Mushi.

Muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo, Magreth Kienzi, amesema jengo jipya la Mama na Mtoto litamaliza changamoto ya msongamano uliopo katika wodi ya wazazi na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma.

Amesema kwa sasa jengo linalotumika ni dogo ukilinganisha na idadi ya wajawazito wanaofika hospitalini hapo, jambo linalosababisha wakati mwingine akina mama wengi kuhudumiwa katika eneo lenye nafasi finyu.

"Jengo jipya litakuwa na eneo la kusubiri wajawazito wanaohitaji uangalizi wa karibu kabla ya kujifungua, na huduma zote muhimu za mama na mtoto zitapatikana katika jengo moja. Hii itarahisisha utoaji wa huduma za haraka na salama kwa mama pamoja na mtoto," amesema Kienzi.

Kukamilika kwa miradi hiyo kunatarajiwa kuongeza uwezo wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama kutoa huduma za kisasa na zenye ubora, huku ikiendelea kuhudumia wakazi wa Manispaa ya Kahama na maeneo jirani.










No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso