Na Neema Nkumbi, Kahama
Diwani wa Kata ya Malunga, Ahmed Haruna, amewapa wamiliki wa vibanda na meza katika Soko la Marunga muda wa miezi mitatu kukamilisha ujenzi wa maeneo yao, akionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo baada ya muda huo kuisha.
Uamuzi huo umefikiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika ndani ya soko hilo ukiongozwa na Diwani huyo pamoja na Mtendaji wa Kata ya Marunga, Bi. Rogath Kimario, kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu kusuasua kwa ujenzi wa vibanda kwa zaidi ya miaka 13, hali inayodaiwa kuchangia kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu na kudumaa kwa shughuli za biashara.
Akizungumza katika mkutano huo, Haruna amesema moja ya vipaumbele alivyovibaini baada ya kuchaguliwa ni kuboresha Soko la Malunga ili liendane na hadhi ya masoko mengine yaliyopo Manispaa ya Kahama.
"Tulipoanza kazi niliona kuna mambo mengi hayako sawa, Tukishirikiana na wananchi wa Malunga kuyarekebisha kata yetu itang'ara zaidi ya ilivyo sasa na moja ya maeneo yanayohitaji mabadiliko ni soko hili," amesema.
Ameeleza kuwa baada ya kufuatilia nyaraka, serikali ilibaini kuwa asilimia kubwa ya vibanda vilivyotolewa tangu mwaka 2013 vinamilikiwa na wananchi wa Kata ya Marunga, lakini wengi wao hawajakamilisha ujenzi licha ya kupewa maeneo hayo kwa lengo la kuendeleza soko.
"Tulipofuatilia nyaraka, tukabaini asilimia kubwa ya waliogawiwa vibanda ni wananchi wa Marunga Tunawaomba kila mwenye kibanda na kila mwenye meza ajenge eneo lake ili soko hili libadilike na lifikie hadhi ya masoko mengine ya Manispaa ya Kahama," amesema.
Diwani huyo amesema baada ya mashauriano yaliyowashirikisha viongozi wa serikali ya mtaa, watendaji na viongozi wengine wa kata, imekubaliwa kutoa muda wa mwisho wa miezi mitatu kwa wamiliki wote kujitokeza kuthibitisha umiliki na kukamilisha ujenzi wa vibanda vyao.
"Kuanzia tarehe 1 Agosti tunaanza kuhesabu miezi mitatu. Baada ya muda huo kuisha Serikali itaingia kwenye hatua ya utekelezaji, Hatutaki baadaye mtu aseme hakujulishwa," amesisitiza.
Aidha, amewataka wamiliki wa vibanda kufika kwa viongozi wa serikali ya mtaa kujaza nyaraka za uthibitisho wa umiliki ili kurahisisha utekelezaji wa maamuzi yatakayochukuliwa baada ya Novemba 30, 2026.
Haruna amesema kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo kutasaidia kuimarisha usalama, kuongeza ajira kwa wananchi, kukuza biashara na kuongeza mapato ya Halmashauri kupitia shughuli za kiuchumi zitakazofanyika katika soko hilo.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo waliunga mkono uamuzi huo, wakisema vibanda na maboma ambayo hayajakamilika vimekuwa maficho ya wahalifu na chanzo cha hofu kwa wananchi, hasa nyakati za usiku.
Mkazi wa Malunga, Boniveture Maganga, amesema hali hiyo imekuwa ikihatarisha usalama wa wananchi na wafanyabiashara wanaopita eneo hilo.
Naye William Mond, Kamanda Mkuu wa Kata, amesema maboma na vichaka vilivyopo ndani ya soko hilo vimechangia kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, hivyo kukamilika kwa ujenzi kutarejesha usalama na kufanya eneo hilo litumike kwa shughuli halali za biashara.
Bi. Sesilia Clement, Afisa Mtendaji Mstaafu wa Kata ya Marunga, amesema inasikitisha kuona mradi wa soko aliouanzisha ukiwa bado haujakamilika baada ya zaidi ya miaka 13, wakati kata nyingine zilizoanzishwa baadaye zimefanikiwa kuwa na masoko yanayofanya kazi kikamilifu.
"Inasikitisha kuona mradi huu umekwama kwa muda mrefu kiasi hiki Kata nyingi mpya zimeendelea, lakini Malunga imeendelea kubaki nyuma kutokana na kutokukamilika kwa soko hili," amesema.
Wananchi pia walipendekeza kuwa wamiliki watakaoshindwa kukamilisha vibanda vyao ndani ya muda uliotolewa wavuliwe umiliki au wauze maeneo hayo kwa watu wenye uwezo wa kuyaendeleza, ili soko lianze kufanya kazi kikamilifu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Kata ya Malunga.








No comments:
Post a Comment