Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama, Joachim Simbila, amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano baada ya uchaguzi mkuu, akieleza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii.
Akizungumza katika mkutano wa kuwashukuru wananchi baada ya uchaguzi uliofanyika Kijiji cha Nyambula Manispaa ya kahama, Simbila amesema wananchi wa Kahama wameonyesha ukomavu wa kisiasa kwa kushiriki uchaguzi kwa utulivu na kufanya maamuzi yao kwa amani, jambo ambalo limeendelea kuifanya Tanzania kuwa mfano wa utulivu barani Afrika.
Simbila amesema bila amani hakuna maendeleo, akibainisha kuwa hata miradi ya maendeleo, biashara na maisha ya wananchi haviwezi kusonga mbele endapo kutakuwa na migogoro na vurugu katika jamii, amesema kila mwananchi ana wajibu wa kuitunza amani iliyopo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, amegusia changamoto zinazoendelea kujitokeza duniani ikiwemo vita katika baadhi ya mataifa, akisema athari zake zinaonekana hata kwa wananchi wa kawaida kupitia kupanda kwa gharama za maisha na changamoto za kiuchumi, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuendelea kulinda amani nchini Tanzania.
Katika hitimisho lake, Katibu huyo wa CCM Wilaya ya Kahama amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na viongozi wao katika kuleta maendeleo, huku akisisitiza kuwa umoja na mshikamano ndiyo nguzo muhimu ya mafanikio ya taifa.

No comments:
Post a Comment