
Mkuu wa kituo cha jeshi la zimamoto na uokoaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga Hafidhi Omari akitoa elimu kwa mtoto Mary Michael ya namna ya kuogelea kwa kutumia jaketi maalumu ili kuzuia majanga, wakati jeshi hilo likifanya kaguzi kinga kwenye kumbi za sterehe na maeneo yenye mikusanyiko wilayani humo.
Na Mwandishi wetu - Kahama
Mkuu wa kituo cha zimamoto na uokoaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga Hafidhi Omari, ameongoza askari wa jeshi hilo kufanya kaguzi kinga maeneo ya kumbi za starehe na sehemu zenye mikusanyiko, kuhakikisha wamiliki na wateja wao wanachukua tahadhari dhidi ya majanga mbalimbali yakiwemo ya moto na maokozi wanaposherekea sikukuu ya pasaka.
Sambamba na hilo, Jeshi hilo pia limefanikiwa kutoa elimu ya majanga hayo na maokozi katika maeneo yaliyofikiwa, kutoa mbinu za kujikinga, pamoja na namna ya kutoa taarifa mapema jeshi la zimamoto na uokoaji kupitia namba 114 yanapotokea majanga kwenye maeneo hayo na hata majumbani kwao.
Miongoni mwa maeneo yaliyofikiwa ni pamoja na maeneo yaliyokuwa na mikusanyiko mkubwa wa watoto wakisherehekea pasaka, ambayo ni KFC, Nitesh, Meru Garden, Yolanda Hotel, Good Valley Hotel na Sindano Hotel.
"Tumetembelea maeneo ya mikusanyiko na kumbi za starehe, kufanya kaguzi kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto na maokozi. Tumetoa elimu ya namna ya kujikinga na maokozi wakati watu wanaposherehekea pasaka, na hata wanapokuwa majumbani nini wafanye kujikinga, namna gani maokozi ya awali yanaweza kufanyika wakati huo huo watoe taarifa kupitia namba 114, ni muhimu sana kabla majanga hayajawa makubwa. Wasipambane kimya kimya."
Omari amesema huo ni utaratibu wa kila mara kwa jeshi hilo kuhakikisha jamii inapata elimu ya kutosha, ili kupunguza majanga yanayoweza kuzuilika, na kurahisisha maokozi pale majanga yanapotokea.
"Tumetembelea maeneo takribani sita, kukagua na kutoa elimu. maeneo mengine tumefanya kaguzi kinga za kawaida na jamii inaendelea kuelimika na kujikinga ambapo mpaka tunatamatisha usiku huu hakuna tukio lolote lililoripotiwa, na bado tupo kazini kuhakikisha jamii inakuwa salama dhidi ya majanga mbalimbali." Amesema Omari na kuongeza
"Tumetembelea zaidi maeneo ambayo yana michezo ya watoto na kuogelea, kwa sababu watoto ni kundi ambalo linahitaji uangalizi mkubwa na elimu, kwa sababu wako kwenye mazingira tofauti na waliyoyazoea ya nyumbani, wanapokuja huku wanahitaji pia wafundishwe namna ya kuwa nje ya nyumbani na walindwe na kujilinda wenyewe, tunashukuru wametuelewa pamoja na wasimamizi wao na wako salama."
Nae mtoto Mary Michael, amesema "Tumefurahi tumefundishwa namna ya kuogelea tukiwa salama mpaka tutakaporudi nyumbani, tunawashukuru sana zimamoto, pia tumejua umuhimu wa kuogelea na hizi jaketi kwa sababu sio rahisi kuzama hata ukichoka au ukianguka kwa bahati mbaya kwenye maji."











No comments:
Post a Comment