VYOMBO VYA ULINZI: MUHIMILI WA AMANI NA MAENDELEO TANZANIA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 6 April 2026

VYOMBO VYA ULINZI: MUHIMILI WA AMANI NA MAENDELEO TANZANIA



Vyombo vya ulinzi na usalama nchini vimeendelea kutajwa kuwa mhimili mkuu wa amani na utulivu wa muda mrefu, hali inayotoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii bila hofu.


Akizungumza katika mahojiano maalumu, Mhadhiri Msaidizi wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Esaka Mugasa, amebainisha kuwa utulivu wa Tanzania si jambo la bahati mbaya, bali ni matokeo ya mfumo imara wa usalama ulioratibiwa kisheria kupitia Baraza la Usalama la Taifa.



Mugasa alifafanua kuwa utendaji kazi wa pamoja kati ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ndio siri ya mafanikio hayo.

Alibainisha kuwa JWTZ lina nafasi ya kipekee si tu katika kulinda mipaka, bali pia katika diplomasia ya kijeshi kupitia misheni za kulinda amani kikanda (SADC) na kimataifa, jambo linalozuia vitisho vya nje kuvuka mipaka ya nchi.

Katika upande wa usalama wa ndani, Jeshi la Polisi limepongezwa kwa kuwa mstari wa mbele katika kulinda maisha na mali za raia. Jitihada za serikali katika kuboresha miundombinu, ikiwemo ujenzi wa vituo vya polisi zaidi ya 470, zimeongeza kasi ya mwitikio dhidi ya uhalifu. Aidha, mfumo wa Polisi Jamii umetajwa kuimarisha uaminifu kati ya raia na vyombo vya dola, hali inayosaidia ugunduzi wa mapema wa viashiria vya uvunjifu wa amani.

Mhadhiri huyo alisisitiza umuhimu wa intelijensia inayofanywa na Idara ya Usalama wa Taifa katika kubaini vitisho kama ugaidi na uhalifu wa kupangwa kabla havijaleta madhara makubwa.

Vilevile, aligusia mchango wa Idara ya Uhamiaji katika kudhibiti biashara haramu ya binadamu na magendo mipakani, huku Jeshi la Magereza likichangia utulivu kupitia programu za kurekebisha tabia za wafungwa ili wasirejee kwenye uhalifu baada ya kutumikia vifungo vyao.

Kwa mtazamo wa baadaye, Mugasa alihimiza uwekezaji zaidi katika teknolojia za kisasa za usalama na elimu kwa umma ili kukabiliana na changamoto zinazoibuka. Alihitimisha kwa kusema kuwa amani ya kweli hailindwi na taasisi pekee, bali hujengwa kupitia mazungumzo jumuishi, umoja wa kitaifa, na uaminifu kati ya serikali na wananchi wake, jambo ambalo litaendelea kuifanya Tanzania kuwa kisiwa cha utulivu barani Afrika.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso