Wito wa kuendelea kudumisha amani nchini umetolewa kwa wananchi, wakihimizwa kutodanganyika na taarifa zinazoweza kuleta taharuki au kupunguza mshikamano wa kitaifa, bali kuendelea kushikamana katika kulinda utulivu uliopo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara, Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (Ccm) Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa amesema Watanzania wanapaswa kuwa makini na baadhi ya watu wanaoweza kutoa kauli za kubeza jitihada za maendeleo zilizofanywa na serikali, ikiwemo ujenzi wa miundombinu muhimu kama madaraja, barabara, maji, umeme na huduma za afya.
Amesema miradi hiyo ni matokeo ya utekelezaji wa sera za Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa huduma hizo zinawanufaisha wananchi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa.
“Tuendelee kulinda amani yetu, wapo watu unaweza ukadanganywa kwamba CCM na Serikali yake hakuna kilichofanyika… lakini ukiona mfano kama daraja limejengwa na serikali, linawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi,” amesema Mabala.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wananchi kuendelea kushiriki kwa amani katika chaguzi na michakato ya kidemokrasia, huku wakihakikisha wanabaki watulivu na kuepuka vurugu zinazoweza kuharibu miundombinu na kurudisha nyuma maendeleo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwaunga mkono viongozi waliochaguliwa pamoja na serikali, akieleza kuwa amani ya nchi ni matokeo ya uongozi thabiti na sera zinazolenga ustawi wa wananchi wote.
Katika ujumbe wake, Mabala amewapongeza wananchi wa Mwabomba kwa kudumisha utulivu wakati wa uchaguzi na kusubiri matokeo kwa amani, akisema tabia hiyo ni mfano mzuri wa uzalendo unaopaswa kuigwa na maeneo mengine.
“Endeleeni kuwa watulivu, endeleeni kuwa wamoja, Amani ndiyo msingi wa maendeleo yetu,” amesisitiza.
Kwa ujumla, wananchi wamehimizwa kuendelea kushikamana, kuepuka uchochezi, na kulinda amani ya nchi ambayo imekuwa msingi muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.

No comments:
Post a Comment