Na Mwandishi Wetu
Wajasiriamali wadogowadogo katika masoko mbalimbali ya Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, wameeleza kuwa amani na utulivu wa nchi ni msingi mkubwa unaowezesha biashara kufanyika kwa mafanikio na wananchi kujipatia kipato cha halali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti sokoni, wafanyabiashara hao wamesema mazingira ya amani huwapa nafasi ya kufanya kazi kwa utulivu, kuhudumia wateja bila hofu, pamoja na kukuza biashara zao hatua kwa hatua.
Bi. Rehema Lazaro, ambaye ni muuzaji wa mboga mboga, amesema kuwa nchi inapokuwa salama, watu hujitokeza kwa wingi sokoni kununua bidhaa na hivyo kuongeza mapato kwa wafanyabiashara.
"Amani ikiwapo, biashara zinaenda vizuri, Watu wanatoka majumbani kwao bila hofu, wanakuja sokoni kununua mahitaji yao na sisi tunapata kipato cha kuendesha familia zetu," amesema.
Kwa upande wake, Bw. Hamis Juma, anayejihusisha na biashara ya Samaki, amesema kuwa vurugu au sintofahamu yoyote huathiri moja kwa moja biashara ndogondogo kwa sababu wateja hupungua na shughuli kusimama.
"Sisi wafanyabiashara wadogo tunategemea kila mteja anayefika sokoni, Ndiyo maana tunasisitiza amani ilindwe kwa nguvu zote," amesema.
Nao baadhi ya mama lishe na wauzaji wa vyakula wameeleza kuwa amani pia huwavutia watu kutoka maeneo mbalimbali kufika sokoni, jambo linaloongeza mzunguko wa fedha na kuchochea uchumi wa eneo husika.
Wajasiriamali hao wamewataka Watanzania kuendelea kuwa na mshikamano, kuheshimu sheria na kushiriki katika shughuli za maendeleo ili kudumisha tunu ya amani ambayo imeendelea kuwa fahari ya taifa.
Wafanyabiashara wadogowadogo Kahama wamesema kuwa bila amani hakuna biashara, na bila biashara hakuna maendeleo ya wananchi wala taifa.

No comments:
Post a Comment