
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu akikabidhi risiti ya benki ya Tsh. Milioni 20,000,000 kwa Padri Didas Nandi, kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Parokia ya Mt. Fransisco wa Asiz iliyopo Msandamungano, mkoani Rukwa, leo Aprili 12, 2026. Pesa hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba,

Katika mkakati kabambe wa kuimarisha mshikamano wa kitaifa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, ametoa wito mzito kwa Taasisi na Viongozi wa Dini nchini kutosimama kando, bali kuwa mstari wa mbele kushirikiana na Serikali kulinda na kudumisha Tunu za Taifa.
Akizungumza mkoani Rukwa, Waziri Sangu amesisitiza kuwa Amani, Upendo, Mshikamano, na Umoja wa Kitaifa ndivyo vishikizo vikuu vinavyolishikilia Taifa la Tanzania, na bila misingi hiyo, ustawi na maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana.
Mabilioni ya Harambee na Ishara ya Umoja
Mhe. Sangu aliyasema hayo alipomwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, katika harambee ya ujenzi wa Kanisa la Parokia ya Mt. Fransisco wa Asizi, Msandamungano iliyofanyika kanisani hapo leo Aprili 12, 2026.
Katika tukio hilo la kihistoria lililojaa hekaheka za kizalendo, zaidi ya Tsh. Milioni 53 zilichangwa, huku Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akionyesha mfano kwa kuchangia Tsh. Milioni 20 taslimu—ishara tosha ya namna Serikali inavyothamini mchango wa taasisi za dini katika ujenzi wa nchi.
Dhamana ya Mahusiano na Dira ya 2050
Waziri Sangu ameweka wazi kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imepewa dhamana nzito ya kuratibu mahusiano kati ya Serikali na makundi ya kijamii ili kuhakikisha maridhiano yanatawala.
Alibainisha kuwa ushirikiano huo umedhihirishwa kwa vitendo kupitia ushirikishwaji wa viongozi wa dini katika kuandaa Dira ya Maendeleo 2050.
"Dhamira yetu ni kuijenga Tanzania tuitakayo kupitia maono ya pamoja. Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua kuwa viongozi wa dini ni nguzo muhimu katika kulea vijana kiroho ili wawe wazalendo, wenye maadili mema na tabia njema zinazochochea jamii tulivu yenye amani," alisema Waziri Sangu.
Rai kwa Waumini na Viongozi
Waziri huyo hakusita kuwasihi waumini kumuunga mkono Rais Samia kwa vitendo, akisisitiza kuwa ujenzi wa taasisi za dini ni sehemu ya maendeleo ya kijamii ambayo Serikali itaendelea kuyaunga mkono.
Alimshukuru Paroko wa Parokia hiyo, Padri Didas Nandi, kwa kuratibu vyema harambee hiyo inayolenga kukusanya jumla ya Tsh. Milioni 900 kwa ajili ya kukamilisha nyumba hiyo ya ibada.
Padri Nandi: Sisi ni Kiungo cha Amani
Kwa upande wake, Padri Didas Aisakus Nandi ameahidi kuwa Kanisa litaendelea kuwa kiungo muhimu kati ya waumini na Serikali. Alisisitiza kuwa juhudi zao za kiroho hazitaishia madhabahuni, bali zitakwenda mitaani kuhamasisha amani, ushirikiano na maendeleo endelevu ili kuhakikisha Tunu za Taifa hazitikisiki.







No comments:
Post a Comment