Baadhi ya vijana wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha amani nchini, wakieleza kuwa utulivu ni msingi wa maendeleo, ajira na ustawi wa jamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, vijana hao wamesema amani hutoa fursa kwa kizazi cha sasa kujenga maisha bora kupitia elimu, biashara na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.
Kijana Zainab Charles amesema vijana wanahitaji kuona taifa lenye mifumo imara inayowapa matumaini ya kesho iliyo bora.
“Tunataka nchi yenye ajira, utulivu na usawa, Haya yote yanaanzia kwenye amani na uongozi unaoweka wananchi mbele,” amesema.
Naye dereva pikipiki ( bodaboda) John Malagala wa Manispaa hiyo wameeleza kuwa wakati wa kipindi cha uchaguzi kulijitokeza changamoto mbalimbali zilizoathiri shughuli za kijamii na kiuchumi, ikiwemo uharibifu wa baadhi ya miundombinu na kusimama kwa huduma katika maeneo kadhaa.
Malagala amesema hali hiyo ilisababisha wananchi kupata shida katika upatikanaji wa huduma muhimu, kufika masokoni na kuendesha shughuli zao za kila siku kutokana na kukosekana kwa utulivu.
Pia wameeleza kuwa sekta ya biashara iliathirika, hususan usafirishaji wa mazao na matunda, jambo lililosababisha upungufu wa bidhaa pamoja na kupanda kwa bei za baadhi ya bidhaa sokoni.
Wamesema kurejea kwa hali ya amani kumewawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao kwa utulivu, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kushiriki katika kulinda amani ili taifa liendelee kusonga mbele.
Vijana hao wameongeza kuwa mchakato wa kujenga maridhiano na mshikamano nchini unatoa nafasi kwa kizazi cha sasa kujifunza umuhimu wa demokrasia, uvumilivu na kuheshimu sheria za nchi.
Wakazi wa Kahama wameitaka jamii kuendelea kuwa na subira, kuimarisha mshikamano na kuunga mkono jitihada zinazolenga kuijenga Tanzania yenye umoja na utulivu wa kudumu.
Wamesema historia ya Tanzania imejengwa juu ya misingi ya amani, na ni wajibu wa kila kizazi kuhakikisha tunailinda hazina hiyo kwa manufaa ya sasa na ya baadaye.

No comments:
Post a Comment