
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, leo amewasilisha ripoti ya tume hiyo kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akifichua kuwa jumla ya watu 518 walipoteza maisha wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa Dar es Salaam ndiyo iliyoongoza kwa vifo 182, ikifuatiwa na Mwanza 90, Mbeya 80, na Arusha 53.
Tume hiyo imebaini kuwa ghasia hizo hazikuwa za bahati mbaya, bali zilipangwa, kuratibiwa, na kufadhiliwa na watu wenye mafunzo maalum waliotumia mbinu 16 tofauti.
Wahusika wakuu wanadaiwa kuwatumia vijana, waendesha pikipiki (bodaboda), na watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapa malipo ya kati ya shilingi 10,000 hadi 50,000 na ahadi za ajira, ili kuanzisha vurugu sehemu mbalimbali kwa wakati mmoja kwa lengo la kuwatawanya nguvu za Jeshi la Polisi.
Aidha, ripoti imeweka wazi kuwa maandamano hayo yalikiuka misingi ya Katiba ya Tanzania, hasa Ibara za 18 na 20, kwani washiriki walibeba silaha na hawakutoa notisi kwa Jeshi la Polisi kama sheria inavyoelekeza.
Jaji Chande ameeleza kuwa kufanya ghasia siku ya uchaguzi ilikuwa ni "kupoka haki ya kikatiba" ya wananchi wengine kushiriki kupiga kura, huku malengo makuu ya vurugu hizo yakitajwa kuwa ni kuvuruga uchaguzi, kufikisha ujumbe kwa Serikali, pamoja na kufanya uporaji wa mali.
Kuhusu sababu za vifo, uchambuzi wa kitaalamu wa maiti 219 (post-mortem) ulibaini kuwa vifo vingi vilitokana na kupoteza damu nyingi, majeraha ya ubongo, na matumizi ya silaha za moto.
Ripoti imetaja tuhuma nzito za watu kupigwa risasi hata katika maeneo ambayo hayakuwa na ghasia, ikiwemo ndani ya nyumba na maduka, jambo ambalo Tume imependekeza lifanyiwe upelelezi wa kina wa kijinai ili kubaini ukiukwaji wa miongozo ya matumizi ya silaha.
Tume imeeleza masikitiko yake kwa vifo vya watoto 21 na pengo kubwa la kiuchumi lililoachwa kwa familia zilizopoteza wategemezi wao.
Pamoja na vifo vilivyorekodiwa, ripoti imebainisha kuwa kuna madai ya watu 39 ambao bado hawajulikani walipo, huku ikionya kuwa idadi ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi kwani baadhi ya majeruhi waliamua kutibiwa katika vituo binafsi bila kutoa taarifa rasmi.
No comments:
Post a Comment