
Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande, amesema ushahidi wa kidijitali uliofanywa na Tume hiyo umebaini kuwa baadhi ya picha mnato na picha mjongeo zilizokuwa zikisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii wakati wa matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 hazikuwa halisi, bali zilikuwa zimechezewa kwa kutumia teknolojia ya akiliunde (AI) ili kuaminisha umma kuwa ni matukio halisi ya maafa na vifo.
Jaji Chande amebainisha hayo leo Alhamisi, Aprili 23, 2026, Ikulu Jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kukabidhi ripoti ya uchunguzi wa Tume hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akitolea mfano wa picha iliyosambaa ikionesha mifuko yenye maiti zikidaiwa kuzikwa kwa halaiki.
Amesema: “Tume tuliweza kutofautisha picha halisi na zisizo halisi kwa kutumia utaalamu, kwa mfano mojawapo ni picha ambayo imetumika mara nyingi kuonesha maiti zikiwa kwenye mifuko ya buluu zikizikwa kwenye makaburi ya halaiki. Picha hiyo kwa mujibu wa uchunguzi imetumika sehemu nyingi duniani.”
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, Tume ilitumia ushahidi na taarifa mseto kutoka katika vyanzo mbalimbali ili kufikia viwango vya uthibitisho vinavyotambuliwa kimataifa, huku ikihakikisha uwepo wa ushahidi wa kujitosheleza.
Ameeleza kuwa katika uchunguzi huo wa kidijitali, Tume ilifanikiwa kukusanya jumla ya picha mnato 450 na picha mjongeo 880 kupitia njia mbalimbali, ikiwemo zile zilizosambaa mara nyingi mtandaoni, zilizowasilishwa na mashahidi, taarifa kutoka vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na vyanzo vya wazi kama vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
No comments:
Post a Comment