Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Bi. Shirley Ayorkor Botchwey. amesisitiza dhamira ya Jumuiya ya Madola kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora na maridhiano ya kitaifa.
Aidha amesema kuwa Jumuiya hiyo inaunga mkono juhudi zinazoendelea nchini na iko tayari kusaidia kujenga mazingira ya kisiasa yenye utulivu, ushirikishwaji na kuaminiana kupitia mazungumzo na mageuzi ya taasisi.
Hayo yamo katika ujumbe wake uliowasilishwa na Mjumbe Maalum na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Malawi, Mhe. Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Ikulu ya Dar es Salaam, leo.
Jumuiya ya Madola imesema kwamba inafuatilia kwa makini matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ikiktaka kushiriki kwa uwazi katika juhudi za kuendeleza majadiliano ya vyama na kuimarisha uwajibikaji wa taasisi.
Akizungumza wakati wa kupokea ujumbe huo, Rais Dkt. Samia amesema Tanzania inaendelea kushughulikia hali hiyo kupitia taasisi zake, akizitaja hatua zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo kuunda Tume Huru ya Uchunguzi kwa lengo la kurejesha utulivu na kuimarisha uwajibikaji.
Amebainisha kuwa matokeo ya Tume hiyo yataongoza hatua zinazofuata ikiwemo uwajibikaji, maridhiano na mageuzi ya taasisi, huku Serikali ikiendelea kusimamia mchakato wa maridhiano kupitia majukwaa ya kisheria na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali.
Kwa upande wake, Mhe. Chakwera ameeleza utayari wa Jumuiya ya Madola kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha utawala wa sheria na mshikamano wa kitaifa.
Dkt. Chakwera amehitimisha ziara yake ya kikazi nchini baada ya kufanya tathmini ya hali ya kisiasa na kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa kisiasa na kitaasisi nchini.





No comments:
Post a Comment