
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa Serikali yake itaendelea kufanya maamuzi yenye tija yanayozingatia takwimu na uhalisia wa namba katika kushughulikia changamoto za Hifadhi ya Ngorongoro.
Akizungumza jana Machi 12, 2026, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma mara baada ya kupokea ripoti za Tume mbili alizounda kutathmini mgogoro wa ardhi na zoezi la uhamaji wa hiari, Rais Samia alisema taarifa hizo zimetoa taswira halisi ya hali ilivyo nyanjani, ikiwemo maeneo ambayo Serikali iliteleza.
“Tumesikia kwamba Serikali tulifanya zoezi kwa nia njema, lakini tulikosea baadhi ya maeneo. Hayo ndio maeneo ya sasa kukaa, kutafakari na kuyarekebisha. Kwa hiyo tutaendelea na hilo zoezi baada ya kufanya marekebisho,” alisema Rais Samia huku akibainisha kuwa lengo ni kupata njia bora ya kisera na kisheria.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume hizo, Dkt. Gerald Mbita, aliwasilisha takwimu zinazoonyesha shinikizo kubwa la kijamii na kiikolojia ndani ya hifadhi hiyo.
Alibainisha kuwa idadi ya watu imeongezeka kwa kasi kutoka watu 8,000 mwaka 1959 hadi kufikia 100,793 mwaka 2022, huku ikitabiriwa kufikia watu 276,651 ifikapo mwaka 2050 kama hatua za makusudi hazitachukuliwa.
Ripoti hiyo pia iligusa upande wa usalama wa binadamu, ikifichua kuwa wastani wa watu saba wamekuwa wakiuawa na wanyamapori kila mwaka kati ya 2015 na 2025, jambo lililosababisha jumla ya vifo 77 na majeraha kwa watu 274. Hali hiyo imeenda sambamba na ongezeko la mifugo iliyofikia 715,466 mwaka 2022, kulinganishwa na mifugo 261,723 pekee iliyokuwepo mwaka 1960.
Athari za mwingiliano huo wa binadamu na wanyama zimeanza kuonekana katika ikolojia ya hifadhi hiyo maarufu duniani. Dkt. Mbita alieleza kuwa utafiti unaonyesha kutoweka kwa baadhi ya wanyamapori kama choroa, nyamela, na swala twiga, huku idadi ya nyumbu wakazi ikipungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu.
Kufuatia ripoti hizo, Tume imeshauri Serikali kuendelea na zoezi la kuwahamisha wakazi kuelekea maeneo yaliyotengwa, lakini kwa kufanya maboresho makubwa katika uratibu, ushirikishwaji wa jamii, na marekebisho ya sheria ili kulinda maslahi ya wananchi na uhifadhi kwa pamoja.
Rais Samia amekubali mapendekezo hayo na kuielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kusimamia utekelezaji wake, huku Katibu Mkuu Kiongozi akipewa jukumu la kuratibu mchakato mzima ili kuhakikisha Ngorongoro inabaki kuwa urithi wa taifa na dunia kwa vizazi vijavyo.
No comments:
Post a Comment