VITA DHIDI YA UCHOCHEZI MITANDAONI: VIJANA SASA WAJITAMBUA, WAHIMIZA AMANI NA MALEZI BORA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 13 March 2026

VITA DHIDI YA UCHOCHEZI MITANDAONI: VIJANA SASA WAJITAMBUA, WAHIMIZA AMANI NA MALEZI BORA




Wakati ulimwengu wa kidijitali ukikabiliwa na changamoto ya kuongezeka kwa jumbe za uchochezi, vijana na wadau wa maendeleo nchini Tanzania wameanza kuonyesha kiwango kikubwa cha kujitambua kwa kutanguliza amani na umoja wa kitaifa mbele ya maslahi ya mitandao ya kijamii.


Hali hiyo imejidhihirisha kupitia maoni ya wadau mbalimbali mkoani Arusha, ambao wamesisitiza kuwa silaha kubwa ya kushinda vishawishi vya vurugu ni elimu ya uraia na msingi imara wa malezi kuanzia ngazi ya familia.


Akizungumzia hali ya amani, mkazi wa Njiro, Angelina William, ametoa rai kwa vijana kuelewa kuwa amani si jambo la bahati mbaya, bali ni hitaji muhimu ambalo lisipokuwepo, jamii nzima huingia kwenye taharuki. Aliongeza kuwa jukumu la kulinda amani linaanza na wazazi katika malezi ya watoto wao.
“Sisi wazazi tunatakiwa kuangalia watoto wetu wamelelewaje. Malezi yakiwa katika mmomonyoko, matokeo yake ni vurugu na mhemuko. Vurugu ni matokeo ya kupwaya kwa suala zima la malezi. Tuna kazi ya kufanya ili watu wajue amani inatengenezwaje kupitia elimu ya uraia,” alisema Angelina.


Naye kijana Hassan Ramadhani Mchome, ameungana na wenzake kupongeza utulivu uliopo nchini, akibainisha kuwa bila amani hakuna kazi wala maendeleo yanayoweza kupatikana. Hassan amewatahadharisha vijana wenzake dhidi ya kufuata mkumbo wa maneno yanayoandikwa kwenye mitandao ya kijamii bila kufanya uchambuzi wa kina.


“Mitandao ya kijamii inaweza kuathiri amani yetu. Tunapaswa kuchambua neno lililoandikwa lina maana gani na tusichukue kila jambo la mtandaoni. Kama vijana, tunaweza kulinda nchi yetu tukiwa na umoja na kushirikiana na viongozi wetu. Rais Samia aendelee kusimamia amani hii,” alisisitiza Hassan.


Kwa upande wake, Afisa Ardhi wa Jiji la Arusha, Adeline Mgele, ameweka msisitizo kuwa amani inaanzia nyumbani kupitia maelewano kati ya baba na mama. Alisema kuwa amani inastawi pale ambapo maslahi ya kila mmoja yanalindwa na uwajibikaji unakuwepo ndani ya familia.


“Amani ndio msingi wa kila kitu; upendo ukitamalaki katika familia na uwajibikaji ukiwepo, maendeleo yanakuja yenyewe. Ni lazima tuhakikishe msingi huu wa amani unalindwa kuanzia ngazi ya chini ili taifa liendelee kuwa imara,” alisema Adeline.


Mageuzi haya ya kifikra miongoni mwa vijana yanatajwa kuwa pigo kwa wachochezi wa mitandaoni ambao wamekuwa wakijaribu kutumia majukwaa hayo kuibua mivutano, huku Watanzania wengi sasa wakionyesha kukomaa kwa kuchuja taarifa na kuthamini utulivu wa nchi yao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso