Na Sheila Katikula, Mwanza
WANANCHI kadhaa katika eneo la Mkuyuni jijini Mwanza wameiomba serikali kuwasaidia baada ya bidhaa zao za biashara na baadhi ya nyumba kusombwa na maji kufuatia mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni na kusababisha mafuriko.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara katika soko la Mkuyuni pamoja na wamiliki wa maduka na nyumba za makazi walisema mvua hizo zimesababisha nafaka zao kulowana na kuharibika, hali iliyowasababishia hasara kubwa na kukata mitaji yao ya biashara.
Katibu wa Soko la Mkuyuni, Simoni Mashamba, alisema soko hilo lina takribani wafanyabiashara 300 na amekuwa akifanya biashara hapo kwa zaidi ya miaka 30.
Alisema ingawa nyakati za mvua maji huwa yanaingia sokoni, haijawahi kutokea maji kuwa mengi kiasi hicho.
Aliiomba serikali kuwasaidia kwani hasara waliyoipata ni kubwa, baada ya nafaka walizokuwa wakiuza kusombwa na maji na kuharibika.
Mfanyabiashara wa nafaka katika soko hilo, Emmanuel Madilisha, alisema maji yaliyoingia sokoni yalikuwa mengi kupita kiasi na kuharibu udaga, mtama, mchele na uwele aliokuwa akiuza.
Alisema hata baada ya kufanya jitihada za kukausha nafaka hizo, haziwezi tena kutumika kwa matumizi ya binadamu.
“Angalia huu mchele na uwele umeanza kuota na unanuka. Vimeharibika kabisa. Udaga nao unanuka, sijui nifanyeje, nimepata hasara kubwa,” alilalamika Madilisha kwa huzuni.
Mfanyabiashara mwingine, Leocardia Masaho, alisema mchele wake mwingi ulisombwa na maji huku uliobaki ukiwa umeharibika na haufai tena kwa matumizi ya chakula, jambo lililomsababishia hasara kubwa.
Aliongeza kuwa ujenzi wa reli ya mwendokasi (SGR) umehusishwa na kuchimbwa kwa ardhi katika eneo hilo, hali iliyosababisha maji ya mvua kupata njia na kumiminika kuelekea sokoni.
Kwa upande wake, Diwani wa kata hiyo, Richard Masesa, alisema viongozi walifika mapema katika eneo hilo na kufanikiwa kuwaokoa baadhi ya wananchi waliokuwa wamepanda juu ya paa za nyumba zao ili kuokoa maisha yao.
Alisema wananchi wengi wamekumbwa na adha ya kubomokewa na nyumba zao huku wafanyabiashara wa nafaka wakipata hasara kubwa baada ya bidhaa zao kuharibika.
Diwani huyo aliongeza kuwa serikali inaendelea kufanya tathmini ili kubaini ukubwa wa hasara iliyosababishwa na mvua hizo. Pia alisema serikali ina mpango wa kujenga soko jipya katika eneo hilo, hatua ambayo anaamini itasaidia kutatua changamoto zinazowakumba wafanyabiashara hao siku zijazo.
Mwisho.


No comments:
Post a Comment