Neema Nkumbi, Shinyanga
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amewataka vijana wa Mkoa wa Shinyanga kuwa washiriki wa maendeleo ya uchumi, si watazamaji wa mambo ya kiuchumi.
Akizungumza leo februari 21, 2026 katika Jukwaa la Vijana mkoani humo, Waziri amesema vijana lazima watumie fursa zinazotolewa na serikali ili kujikwamua kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika ukuaji wa mji na taifa.
“Vijana hawapaswi kuwa watazamaji wa mambo ya uchumi, bali wawe washiriki wakuu, Kwa kutumia fursa za mikopo, ujuzi na teknolojia, mnaweza kuanzisha viwanda vidogo vidogo, kujenga mitandao ya biashara, na kujikwamua kiuchumi,” amesisitiza Nanauka.
Ameongeza kuwa mikataba zaidi ya 7 imeingiwa kwa ajili ya kuwapeleka vijana kufanya kazi nje ya nchi, na kwamba shilingi bilioni 200 zilizotolewa na Rais tayari zinaanza kutumika kama mtaji kwa vijana waliojiandaa.
Salamu za Ukaribisho na Takwimu za Vijana
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita amesema mkoa una vijana zaidi ya laki 6.9 na kwamba vijana wamekuwa kipaumbele katika ajenda ya maendeleo ya kiuchumi ambapo amesisitiza umuhimu wa elimu, ujasiriamali, na miongozo ya kisera, huku akibainisha kuwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa imefanikiwa kusajili zaidi ya wajasiriamali 2,000.
Fursa za Mikopo na Uwezeshaji
Vijana wanahimizwa kuchangamkia mikopo ya serikali, ikiwemo ile ya asilimia 10, huku zaidi ya bilioni 2 zikitolewa mwaka wa fedha 2024/2025 katika mkoa wa shinyanga, Aidha, zaidi ya bilioni 5 zimetolewa kupitia Mfuko wa Utamaduni kusaidia vijana wenye vipaji na ubunifu.
Nanauka amesisitiza umuhimu wa nidhamu ya muda, uthubutu, na kuepuka watu wenye maneno hasi. “Ndoto yako ndiyo mtaji wako, Ukiamua jambo lako, usikubali kuyumbishwa. Mafanikio ni fursa kwa aliyejiandaa,” ameongeza.
Wito kwa Vijana
Waziri amewataka vijana kuwa wamoja, kudumisha amani, na kutumia kila fursa iliyofunguliwa na serikali. “Vijana, changamkieni fursa, jumuikeni, na mje na ujasiri, Hivyo tuweze kujenga taifa letu kwa kushirikiana na kuonyesha vipaji vyenu,” amesema.
Moja wa vijana aliyehudhuria jukwaa hilo Elina Evodius amesema amepokea kwa bashaha sana jukwa hili kwani walikuwa wanakosa mahali pa kusemea changamoto zao, pia kupitia jukwaa hili wataweza kupata fedha za mkopo na kujikwamua kiuchumi kwani tayari walishaanzisha kikundi ambacho ni klabu ya mazingira ambapo wanaenda kuanzisha vitalu vya miche mbalimbali ndani ya manispaa ya shinyanga.
Kijana mwingine Ebeneza John amesema akipata fedha hizo za mikopo zitamsaidia katika shughuli zake za kiuchumi hususani katika biashara zake





















No comments:
Post a Comment