KATIKA ulimwengu unaokwenda kasi mithili ya mwanga, ambapo teknolojia imetawala kila nyanja ya maisha, jamii imeaswa kutofanya makosa ya kuzika utu na maadili ya kale.
Rai hiyo imekuja kama radi, ikiwataka vijana wa kizazi cha sasa, maarufu kama 'Gen Z', kusitisha mwendo wao kwa muda na kutazama nyuma kwenye nyayo za mababu zao ili kupata dira ya kweli ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni.
Akizungumza kwa msisitizo mkubwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mabadiliko ya Hatua kwa Hatua ya Binadamu (Anthropolojia), mdau wa masuala ya kijamii, Marian Gichan, ametoa onyo kali dhidi ya mmomonyoko wa maadili unaofichwa nyuma ya kichaka cha usasa.
Gichan amebainisha kuwa, ingawa vifaa vya kisasa na mtandao vimerahisisha mawasiliano, vimeshindwa kuziba pengo la nidhamu, heshima, na utu ambavyo ndivyo vilikuwa uti wa mgongo wa jamii imara ya Wahenga.
"Maendeleo bila maadili ni sawa na nyumba iliyojengwa juu ya mchanga; haihitaji dhoruba kali ili kuanguka," alisisitiza Gichan.
Alifafanua kuwa miiko na simulizi za kale zilizokuwa zikitolewa na wazee chini ya miti au pembeni ya moto wa jioni, hazikuwa hadithi za kusadikika, bali zilikuwa ni kanuni za kisheria na kimaadili zilizolenga kumlinda mwanadamu dhidi ya tamaa na uasi. Kwa mujibu wa Gichan, vijana wa leo wanapaswa kuelewa kuwa heshima kwa wakubwa na nidhamu ya kazi si mambo ya kizamani, bali ni nyenzo muhimu zinazoweza kuwasaidia kuvuka vikwazo vya soko la ajira na mahusiano ya kijamii katika karne ya 21.
Hali kadhalika migongano ya kifikra kati ya vizazi (generation gap) isichukuliwe kama tiketi ya vijana kujitenga na asili yao. Badala yake, tofauti hizo zinapaswa kuwa daraja la kubadilishana maarifa; ambapo kijana anatoa ujuzi wa kidijitali na mzee anatoa hekima ya maisha.
Gichan amewahimiza Gen Z kuchuja kwa umakini yale mema kutoka kwa vizazi vilivyotangulia na kuyapandikiza kwenye ulimwengu wao wa sasa, ili kutengeneza mchanganyiko imara wa maarifa na maadili utakaostahimili dhoruba za utandawazi.
Wadau wa elimu na malezi kwa sasa wanatakiwa kuhakikisha kuwa somo la anthropolojia na historia ya jamii halibaki kwenye vitabu pekee, bali linaishi katika matendo ya kila siku. Ni dhahiri kuwa bila kurejea kwenye misingi ya Wahenga, safari ya kuelekea uchumi wa kati na maendeleo ya kweli itabaki kuwa ndoto ya mchana, huku jamii ikizidi kupoteza utambulisho wake muhimu ulimwenguni.

No comments:
Post a Comment