Na Neema Nkumbi, Kahama
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kuboresha mifumo yake ya ukusanyaji na usimamizi wa kodi kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa IDRAS (Integrated Domestic Revenue Administration System), unaolenga kuongeza ufanisi, uwazi na kupunguza mianya ya upotevu wa mapato ya serikali.
Mfumo wa IDRAS umebuniwa kuunganisha huduma mbalimbali za kodi chini ya mfumo mmoja, hivyo kuwawezesha walipa kodi kujisajili, kukadiria, kulipa kodi na kufuatilia taarifa zao kwa njia ya mtandao bila usumbufu.
Akizungumza kuhusu mfumo huo, Afisa msimamizi wa kodi idara ya elimu na mawasiliano mkoa wa kikodi Kahama Hamis Sanze amesema IDRAS imewezesha:
Kurahisisha usajili wa walipa kodi na utoaji wa TIN
Uwasilishaji wa makadirio ya kodi na marejesho (returns) kwa njia ya mtandao
Malipo ya kodi kwa haraka kupitia benki na mifumo ya kielektroniki
Kupunguza mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mlipa kodi na mtumishi, hivyo kuimarisha uwazi
TRA imewahimiza wafanyabiashara, taasisi na wananchi wote kuhakikisha wanatumia mfumo huo ipasavyo ili kutimiza wajibu wao wa kikodi kwa hiari na kwa wakati.
Kwa mujibu wa Hamis, matumizi ya IDRAS ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa mageuzi ya mifumo ya kifedha na ukusanyaji wa mapato, unaolenga kukuza uchumi na kuongeza uwezo wa serikali kutoa huduma bora kwa wananchi.
Naye mfanya biashara Chona Daniel amesema mfumo huu utawarahisishia wafanya wafanya biashara kuingia kwenye mfumo na kuangalia taarifa zao hivyo hatuna haja ya kwenda TRA kila siku bali tutaenselea kufanya kazi zetu kwa amani.
"Kwa mfano mimi naishi halmashauri ya ushetu ilikuwa inanibidi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za TRA ila kwa sasa mfumo huu umeturahisishia na kutupunguzia gharama za usafiri hivyo tutafanya kazi bila kupoteza muda", amesema Chona.







No comments:
Post a Comment