MONGELLA: HAKI ZA MSINGI NA AMANI NI MSINGI WA MAENDELEO YA TAIFA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 31 January 2026

MONGELLA: HAKI ZA MSINGI NA AMANI NI MSINGI WA MAENDELEO YA TAIFA



Na Neema Nkumbi, Kahama

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, John Mongella, amesema kuwa haki kwa Watanzania haipaswi kuangaliwa kwa mtazamo wa vibali vya mikutano ya hadhara au maandamano pekee, bali kwa upana wake unaojumuisha haki ya kila Mtanzania kuishi maisha bora katika jamii yenye ustawi.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 49 ya CCM Wilayani Kahama, Mongella amesema Watanzania wengi wanalia kuhitaji haki za msingi ikiwemo uhuru wa kuishi kwa amani, kupata huduma bora za afya, maji safi na salama, elimu bora pamoja na uhuru wa kuabudu, akisisitiza kuwa haki hizo haziwezi kupatikana bila kuwepo kwa amani na utulivu.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kusimamia misingi hiyo ya haki na amani wakati wote, hatua iliyowezesha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo sekta ya elimu.

Mongella ameeleza kuwa Rais Samia amezindua mpango wa elimu wa kisayansi unaolenga kuwawezesha watoto wa Kitanzania kuwa na umahiri wa kusoma na kuandika, ambao ni msingi muhimu wa elimu bora.

Kwa mujibu wa Mongella, siku 100 za mwanzo za Serikali ya Awamu ya Sita zimeonesha dalili chanya za kuimarika kwa amani, utulivu na ustawi wa jamii, hali inayowezesha kila Mtanzania kufurahia haki zake za msingi.

Ametoa wito kwa wanachama wa CCM kutotumia maadhimisho ya miaka 49 ya chama kama sherehe tu, bali kuyatumia kama fursa ya kwenda kwa wananchi kueleza mafanikio yaliyopatikana chini ya serikali za CCM katika awamu zote sita, huku wakitetea haki za wananchi na kuendeleza misingi ya amani, umoja na mshikamano.

Aidha, Mongella amesema CCM kama chama tawala kina wajibu mkubwa wa kuongoza jamii yote ya Watanzania, akisisitiza kuwa viongozi wa chama hawawajibiki kwa wanachama pekee bali kwa taifa zima.

“Niwashauri wenzangu tusibaki katika kusherehekea ushindi wa uchaguzi, bali turudi kazini, Rais wetu alitangaza siku 100 za mwanzo na tumeona akifanya kazi kwa juhudi kubwa, hivyo ni wajibu wa wabunge, madiwani na viongozi wa chama kurejea kwa wananchi na kufanya kazi,” amesema Mongella.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amesema chama mkoani humo kimepokea maelekezo yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu huyo na kumhakikishia kuwa yatafanyiwa kazi kwa vitendo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso