Katika ulimwengu wa usalama wa mtandao, kuna mchezo wa "paka na panya" unaoendelea kati ya mifumo imara ya ulinzi na matapeli wa kidijitali. Hivi karibuni, kumezuka matangazo ya uongo yanayotumia jina la kampuni ya Bakhresa Group yakiahidi "Zawadi Maalum ya Ramadhani," jambo ambalo uongozi wa makampuni hayo umekanusha vikali kuhusika nalo.
Ukweli ni kwamba, ikiwa kampuni yenyewe inasema "si sisi," basi ujue kuna watu wenye nia ovu ambao wana shida na wewe, data zako, au fedha zako.
Inashangaza kuona kuwa unapojaribu kufungua link hizi kupitia kompyuta zenye ulinzi imara na programu za kuzuia virusi (antivirus), mara nyingi unakutana na ujumbe wa "Error 404" au tovuti kuzuiliwa kabisa. Hii ni kwa sababu mifumo ya kompyuta ina uwezo mkubwa wa kuchambua na kubaini kuwa tovuti hizo (kama ile ya heht.kcaeb.xyz) haina usalama (SSL certificate) na ni ya kitapeli. Kompyuta inakupa "Error" kama kinga, ikikuambia kuwa hapa hakuna kitu cha kweli bali ni shimo la hatari.
Hata hivyo, mtego huu unakuwa hatari zaidi unapoingia kwenye "vibatari" au simu za mkononi. Kwenye simu, matapeli wanatengeneza kurasa zinazofanana na "game" au michezo fulani ya kubahatisha, ambapo mtumiaji anahimizwa kubonyeza ili "ashinde". Simu nyingi hazina ulinzi wa ziada kama wa kompyuta, hivyo mtumiaji anajikuta anatoa taarifa zake binafsi au kusambaza mtego huo kwa wengine kwa urahisi, akiamini ni bahati nasibu ya kweli.
Uongozi wa Bakhresa Group umetoa onyo kali kwa wale wote wanaotengeneza au kusambaza matangazo hayo ya uongo, ukiahidi kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yao.
Ni muhimu kwa umma kuelewa kuwa zawadi yoyote inayokuja kupitia tovuti za ajabu zisizo rasmi ni utapeli. Unapoona kompyuta yako inakataa kutoa ushirikiano, chukua hiyo kama ishara ya kwanza; usikimbilie kwenye simu yako kujaribu "bahati" ambayo mwisho wake ni kupoteza faragha na usalama wako wa kidijitali.
No comments:
Post a Comment