Wakati neema ya Sh bilioni 200 ikiwashukia vijana , sauti za wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini zimesisitiza kuwa amani ndiyo mhimili mkuu uliowezesha mabilioni haya kupatikana na kuanza kugawanywa kwa walengwa.
Wakazi wa Bariadi mkoani Simiyu wamekumbusha kuwa bila amani na utulivu, hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana, wakitolea mfano wa adha walizopitia nyakati za vurugu ambazo ziliwalazimu kufanya kazi kwa muda mfupi na kupoteza kipato. Imeelezwa kuwa amani ni mboni ya jicho inayopaswa kulindwa na kila mmoja, kwani hata ndani ya familia, kukosekana kwa amani husababisha watoto kuhangaika mitaani na kila kitu kukwama. Viongozi wamehimizwa kuendelea kusikiliza malalamiko ya watu wao ili kuziba mianya inayoweza kuhatarisha utulivu wa taifa.
Sambamba na kulinda amani, suala la maadili kwa vijana limetajwa kuwa kipaumbele ili kujenga jamii yenye mshikamano itakayoweza kutumia mitaji hiyo kwa tija.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ameitaka jamii kuwekeza nguvu katika kudumisha amani na kusimamia maadili ya dini kwa vijana ili waweze kuwa watu imara katika maendeleo ya Taifa.
Alisisitiza kuwa ni wajibu wa wazazi na wasimamizi kuhakikisha vijana wanapata elimu inayostahiki ya maadili, akibainisha kuwa kila mchunga ataulizwa kwa alichokichunga.
Katika kufikia maendeleo ya kweli, jamii imehimizwa kuwaunga mkono viongozi wakuu wa nchi bila kujali tofauti za dini au vyama, ili kuwapa ari ya kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kuwaletea wananchi maendeleo.
Serikali imetoa mwelekeo mpya kwa kuagiza taasisi za fedha zinazoshirikiana na serikali kuondoa masharti magumu na urasimu usio na tija ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo hii ya mitaji.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesisitiza kuwa mafanikio ya fedha hizi hayatapimwa kwa idadi ya tarakimu bali kwa mabadiliko ya kweli ya maisha ya vijana, akizitaka benki kupunguza kurasa za mikataba zinazotisha wakopaji wadogo.
Wakati mkoa wa Tanga ukichagua amani bila kujali tofauti zilizopo, jitihada hizi za serikali za kuchanganya mitaji, amani, na maadili zinakwenda kuzika rasmi kisingizio cha kukosa mtaji na kufungua milango ya neema kwa vijana wa Kitanzania.
No comments:
Post a Comment