
Katika ulimwengu wa sasa uliotawaliwa na kasi ya kidijitali, kauli ya hivi karibuni ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, imekuja wakati muafaka.
Akizungumza Februari 27, 2026, Waziri ameweka wazi kuwa mustakabali wa sekta ya mawasiliano nchini unategemea mambo makuu matatu: weledi, maadili, na ubora wa huduma. Hata hivyo, kiini cha ujumbe wake kinalenga zaidi jinsi teknolojia inavyopaswa kuwa nyenzo ya maendeleo badala ya kuwa kichocheo cha mmomonyoko wa maadili.
Kwa kauli yake serikali imedhihirisha nia yake ya dhati ya kuhakikisha kuwa miundombinu ya kidijitali inatumika kama daraja la maarifa. Kupitia maelekezo ya Waziri Kairuki, wizara imejipanga kuimarisha usimamizi wa rasilimali na kuongeza kasi ya uwekezaji kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma. Lengo si kutoa intaneti tu, bali kutoa intaneti salama.
Kampeni kabambe inayotarajiwa kufanyika kupitia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara kuelimisha wananchi kuhusu fursa na hatari za kidijitali na kuhakikisha taasisi zinazosimamia mitandao zinatenda kazi kwa uadilifu kuzuia uhalifu wa kimtandao kutasaidia kuandaa vijana wa Kitanzania wenye ujuzi wa kusimamia miradi ya kimkakati na kulinda usalama wa taarifa.
Pamoja na jitihada hizi, kuna ukweli mchungu unaopaswa kusemwa; sehemu kubwa ya vijana na wananchi kwa ujumla wamegeuza mitandao kuwa uwanja wa matumizi yasiyo na tija. Badala ya kutumia majukwaa haya kwa ajili ya kujifunza ujuzi mpya (e-learning), kufanya biashara, au kutafuta taarifa za kimaendeleo, wengi wamezama kwenye ueneaji wa uzushi, kejeli, na maudhui yanayokiuka maadili ya Kitanzania.
Hali hii kiukweli inatishia jitihada za serikali za kuziba pengo la kidijitali kati ya mijini na vijijini, kwani teknolojia inapotumiwa vibaya, inakuwa mzigo badala ya fursa.
"Misingi imara ya maendeleo inajengwa kupitia uongozi thabiti na usimamizi bora wa rasilimali za umma," alisisitiza Mhe. Kairuki. Kauli hii ni agizo kwa kila mdau—kuanzia ngazi ya familia hadi taasisi za elimu—kuhakikisha kuwa mtumiaji wa mtandao anakuwa na nidhamu ya kidijitali.
Kuelekea kilele cha mapinduzi ya nne ya viwanda, usalama wa mtandao si jambo la hiyari bali ni lazima. Ikiwa tutazingatia maelekezo ya Waziri kuhusu weledi na uadilifu, tunaweza kuifanya mitandao kuwa darasa kubwa zaidi duniani kwa ajili ya vijana wetu. Ni wakati wa kila mwananchi kujiuliza: Je, simu yangu ni silaha ya uharibifu au ni nyenzo ya kunikwamua kiuchumi?
No comments:
Post a Comment