SAMIA AWASAMEHE VIJANA WA 'MKUMBO', ATOA WITO MZITO WA KULINDA AMANI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 15 November 2025

SAMIA AWASAMEHE VIJANA WA 'MKUMBO', ATOA WITO MZITO WA KULINDA AMANI



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito mzito kwa vijana wa taifa kuilinda amani ya nchi na kukataa kwa nguvu zote kushawishiwa kuingia kwenye vitendo vinavyohatarisha utulivu wa Tanzania.

Akihutubia Bunge la 13 jijini Dodoma , Ijumaa Novemba 14, 2025, Dkt. Samia alitoa ujumbe wa upatanishi na msamaha, huku akisisitiza kuwa vijana ndio walinzi na wajenzi wa taifa, hivyo hawapaswi kutumia mikono yao kuivunja nchi iliyojengwa kwa amani, jasho na uvumilivu.

“Msikubali kukata tawi la mti mnaoukalia. Msikubali kushawishiwa kuichoma Tanzania. Nyinyi ndio walinzi wa Taifa hili, wajenzi wa kesho yake, kamwe msije kuwa wabomoaji,” alisema Rais Samia, akipokea shangwe kutoka Bungeni.

Katika wito huo huo wa kujenga umoja na matumaini, Dkt. Samia alitangaza hatua kubwa ya msamaha, akielekeza Ofisi ya Mashtaka (DPP) kuwafutia makosa vijana wote waliojiingiza katika vurugu za Oktoba 29, 2025, kwa kufuata mkumbo na ushabiki bila dhamira ya kufanya uhalifu.

“Nikiwa mama na mlezi wa Taifa hili, ninaviomba vyombo vya sheria na hasa Mkurugenzi wa Mashtaka kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana wetu. Kwa wale ambao walijiingiza kwa mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu, wasamehewe,” alisisitiza kiongozi huyo.

Alifafanua kuwa ushahidi wa video unaonyesha wazi kuwa baadhi ya vijana hawakujua uzito wa walichokuwa wakifanya. Akitoa rejea ya kiroho, Rais Samia alikumbusha, “Natoa msamaha huu kwa sababu hata maneno ya Mwenyezi Mungu katika Kitabu cha Luka 23:34 yanasema ‘Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo.’”

Rais Samia alihitimisha kwa kuwakumbusha Watanzania kutanguliza maelewano, ushirikishwaji, na umoja katika safari ya kuelekea miaka mitano ijayo ya Serikali ya Awamu ya Sita, akisisitiza kuwa taifa linahitaji vijana wenye uelewa, walio tayari kujenga badala ya kubomoa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso