TUME MAALUM KUCHUNGUZA VURUGU - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 15 November 2025

TUME MAALUM KUCHUNGUZA VURUGU



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imeunda Tume Maalumu kuchunguza kwa kina kilichosababisha vurugu za Oktoba 29, 2025, akilenga kupata ukweli na kuelekeza Taifa kwenye hatua za maelewano, maridhiano, na amani ya kudumu.

Akitoa hotuba katika uzinduzi wa Bunge la 13, jijini Dodoma, Ijumaa, Novemba 14, 2025, Dkt. Samia alianza kwa kutoa pole za dhati na kuomboleza vifo na majeraha yaliyotokana na tukio hilo la kusikitisha.

“Nimehuzunishwa sana na tukio lile. Natoa pole kwa familia zote zilizopoteza ndugu na jamaa. Tunaomba Mungu aziweke roho zao mahali pema. Kwa majeruhi, tunawaombea wapone haraka, na kwa waliopoteza mali, tunawaomba wawe na stahamala na uvumilivu,” alisema Rais Samia, huku akiwaomba Wabunge na wageni waalikwa kusimama kwa dakika moja kuwaombea waliofariki.

Rais Samia alisisitiza kuwa Serikali haitapuuza kilichotokea, bali itachukua hatua za haki na busara kulinda utulivu wa taifa.

Alieleza kuwa ripoti ya Tume hiyo ndiyo itakayotoa mwongozo wa hatua zitakazochukuliwa, na itasaidia kuongoza jitihada za Serikali katika kujenga maelewano ya kijamii, kutibu majeraha, na kuimarisha misingi ya amani ambayo Watanzania wamerithi kwa vizazi. Hatua hiyo inaonyesha dhamira ya Serikali ya kuweka ukweli mbele ili kuendeleza mwelekeo wa "Kazi na Utu" kwa Taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso